HOME

(5)

 

BARUA YA WAZI  KWA  MAWAHABI

 

Katika karatasi yetu ya nne tuliona mbinu na hila mbalimbali ambazo Muawiya alizitumia kumpatia mwanawe, Yazid, utawala. Alitumia ulaghai, hadaa, uswalata, hongo mpaka vitisho na mabavu! Mwisho, baada ya mbinu zote kushindwa, aliita mkutano wa hadhara.

 

Kwenye mkutano huo, kama alivyowaonya kina Imam Hussein a.s., alipanda juu ya mimbari akasema, “Shuhudieni kuwa hawa waliokuwa wakipinga, sasa wameridhia. Na wenyewe hawa wote wako hapa. Na hawa ndio wazalendo wa Madina na wa Kisahaba. Hakuna lililosalia tenaHivyo ndivyo anavyoeleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29 wa kitabu chake; na akaendelea kuandika, “Akatoa hapo mafedha kwa mafedha kuwapa kila wakubwa wa kila qabila za Kimuhajiri na Ansari na nyinginezo…” Na hivyo ndivyo Yazid alivyopatiwa utawala katika mwezi wa Rajab, mwaka wa 60 BH, baada ya babake kufa.

 

Ewe ndugu Mwislamu! Ikiwa mambo yalikwenda hivyo, kama yalivyoelezwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy, kweli Mwislamu yoyote anayeujua Uislamu wake, na anayetaka kubakisha jina jema la Uislamu, anaweza kujifakhiri kuwa mtu kama Yazid alikuwa ni kati ya viongozi wake wa Kiislamu, sambe (seuze) kumkubali kuwa ni Amiirul mu’minin?! Lakini hayo si aliyoyafanya Yazid, yeye mwenyewe; ni aliyofanyiwa na babake, Muawiya. Aliyoyafanya yeye mwenyewe, baada ya kutawala, ni makubwa zaidi! Ni yapi?

 

Kwa ufupi, anavyotueleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29-41 wa kitabu chake hicho, alifanya yafuatayo:

 

1. Alimpelekea habari Liwali wake wa Madina wa wakati huo, naye ni Khalid bin Hakam, awaapishe mabwana hawa: Huseyn bin Ali bin Abi Talib, Abdalla bin Umar bin Al Khattab, Abdalla bin Al Abbas na Abdalla bin Zubeir. (Abdur Rahman bin Abi Bakr hakuwamo; alikuwa ashakufa). Alimwamrisha “awaapishe yamini kali kabisa kuwa wamekwisha mkubali Yazidi kuwa ndiye Khalifa wa Waislamu wote. Na kuwa wakenda kinyume naye mali yao yawe halali yake, wake zao waachike. Na watumwa wao wawe mahuru

 

2. Liwali huyo alipoweta Imam Hussein a.s. na Abdalla bin Zubeir, waliomba waachwe mpaka siku ya pili. “Kufika majumbani mwao tu”, Sheikh Abdalla anaeleza (uk.30),“waliwaaga watu wao wakatoka kwa siri kwenda Makka kukaa huko kwani mwenye kuweko huko huwa katika amani…” Yazidi, kupata habari hiyo tu, alihamaki “akamtoa( Liwali huyo) katika Uliwali wake.”

 

3. Alipotawala Yazid, kimabavu kama tulivyokwisha kuona, watu wa Al Kufa (Iraq) walimpelekea Imam Hussein a.s. “mabarua ya kumhimiza ende huko Iraq azatiti vita huko kumuondoa huyo asiyestahiki kuwa Khalifa wa Waislamu”. Hata hivyo, Imam Hussein a.s. hakwenda papo hapo, bali alimtuma binami yake (Muslim bin Aqyl) ende huko ili amjulishe ukweli wa mambo ulivyo. Alipopata habari hiyo, Sheikh Abdalla anatueleza (uk 34-35), Yazid “alimchagua Liwali qatili,dhalimu, jabbar, shujaa anayemchukia Sayyidna Ali na kizazi chake, aliyekuwa akiitwa Ubeidillah bin Ziyad ambaye baba yake alithibitishwa na…. Muawiya -- kwa siyasa tu -- kuwa ndugu yake. Akatiwa katika kabila yake ya Bani Umayya hali ya kuwa hakhusiani naye hata chembe, wala hakhusu Uqureshi hata kidogo, bali wala Uwarabu. Ni mtu mwanaharamu tu aliyekuwa hodari sana hata akampinga Muawiya kweli kweli. Akaona amthibitishe kuwa ndugu yake na amwachie amri ya Iraqi yote". Hivyo akawa mwana haramu wa kwanza, katika historia ya Uislamu, kufanywa mwana halali!

 

4. Baada ya kumchagua Liwali huyo, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 35), Yazid alimpa amri hii: "Muuwe huyu Muslim bin Aqyl, na kila waliokuja pamoja naye, na kila waliompokea, na kila walio pamoja naye; na mfunge umuadhibu jamaa na jirani wa kila mmoja katika hawa, usiwe na huruma na yeyote." Na hivyo khaswa ndivyo ilivyokuwa. "Alifanya kama alivyoamrishwa na Yazid, akawamaliza hao wote alioamrishwa awaue, na akawafunga hao alioamrishwa awafunge…"

 

Katika kitabu chake, Sheikh Abdalla S. Farsy hakueleza jinsi alivyouliwa Muslim bin Aqyl. Lakini vitabu vyengine vya historia vinaeleza kwamba alichukuliwa mpaka juu ya kasri moja, akakatwa kichwa ambacho kilitupwa chini kikifuatishwa na pingiti lake. Baadaye kichwa hicho kikapelekwa kwa Yazid!

 

5. Kama tulivyokwisha kuona katika karatasi yetu Na.1, baada ya Imam Hussein a.s. na aliokuwa nao kuuwawa kikatili na kukatwa vichwa vyao, Yazid (alipopelekewa vichwa hivyo) alikamata kifimbo, Sheikh Abdalla S. Farsy anatueleza (uk 40), "akawa anayagonga meno ya Huseyn na kuimba kusema, ' Nimemlipa leo Muhammad ! Kama alivyoniuliya wazee wangu siku ya Vita vya Badr, leo nimemuulia wajukuu wake. Na huu ndio mwendo wetu utakaokuwa. Kila anayetupinga tutamwua japokuwa anatukhusu…"

 

Ewe ndugu Mwislamu! Hebu jiulize: Mtu anayejasiri kusema kuwa anamlipa kisasi Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa kuwauwa makafiri (waliokuwa babu zake yeye Yazid) hufaa au huweza kuitwa Amiirul-mu'minin? Acha hilo! Huweza hata kuitwa Mwislamu? Hivi hao mawahabi wetu hawakulijua hilo? Au watatwambia kuwa Sheikh Abdalla Saleh Farsy alikuwa Shia?

 

Kuna yaliyobaki, na si madogo! Inshallah hayo tutayamaliza katika karatasi ijayo

 

 

ABDILAHI NASSIR,      8 Swafar, 1424

S.L.P. 84603          11 Aprili, 2003

MOMBASA             (Inaendelea)