HOME

(4)

 

BARUA  YA  WAZI  KWA  MAWAHABI

 

Katika karatasi yetu ya tatu tulionyesha, kwa ushahidi wa maneno ya Sheikh Abdalla S. Farsy, jinsi Muawiya alivyotumia njama, vitisho na hongo kumtawalisha mwanawe (Yazid). Lakini mbinu zote hizo hazikufaa kitu. Ndipo pale alipowaandikia wale mabwana wane wa Madina, tuliowataja katika karatasi yetu Na. 3, barua kali za kuwaonya.

 

Walipozipata barua hizo, mabwana hao (anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 24) walimjibu "kwa maneno makali kabisa na tahadidi kubwa kabisa. Na aliyemwandikia maneno mengi kabisa ni Sayyidnal Huseyn."

 

Alipozipata jawabu zao hizo, Muawiya alimwambia tena huyo Liwali wake "azidi kuwalazimisha kwa tashdidi kubwa zaidi kabisa. Akafanya", Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk. 24), "zisifae kitu." Kwa hivyo akamwandikia Muawiya ende tena huko Madina akaonane nao yeye mwenyewe.

 

Alipofika Madina, na "baada ya kupumzika", Sheikh Abdalla anasema (uk. 25), Muawiya "aliwaita kila mmoja akamsemeza siri peke yake ili wasimjibu wote kwa jawabu moja." Wa kwanza alikuwa ni Imam Hussein a.s. "Akamwambia, 'Mwanangu! Usiutilie fujo uma wa babu yako. Watu wote wamekwisha kuridhia kuwa Yazid awe Khalifa baada yangu. Hakuna wanaopinga ila nyinyi tu, na wewe ndiye unayewaongoza. Ukikubali wewe na wao wataridhia, kama walivyonambia.' (Imam Hussein a.s.) akamwambia, 'Wete mbele yangu hapa waseme hayo. Mimi sisadiki kuwa wamesema hivyo. Wakikiri mbele yetu hapa na mimi nitakuwa pamoja nao. Lakini nina yakini kuwa hawatakiri.' Akamwambia, "Basi nenda zako. Lakini usimhadithie yo yote lo lote katika tuliyoyasema." Hivyo ndivyo alivyoandika Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 25 wa kitabu chake hicho.

 

Baada ya Imam Hussein a.s., alimwita Bwana Abdalla bin Zubeir, kisha Bwana Abdulla bin Umar bin Al Khattab. Nao wakamjibu kama alivyojibu Imam Hussein a.s. "neno kwa neno". Hapo tena, Sheikh Abdalla anasema (uk. 25 -- 26), "akapeleka mtu kumwita Bwana Abdur Rahman bin Aby Bakrinis Sidiqq. Akamsemesha maneno makali kabisa na yeye akamjibu makali kabisa. Wakaghadhibishana kweli kweli kwani yeye alikuwa mtu mzima kama yeye."

 

Baada ya hapo ilimbidi Muawiya abadilishe mbinu. Kwa hivyo "siku ya pili", Sheikh Abdalla anasema (uk. 26), " akapeleka mtu kumwita Sayyidnal Huseyn bin Ali na Bwana Abdalla bin Abbas." Baada ya kuzungumza nao "mambo ya hali zao na hali za majumbani mwao", aliingia "kumsifu mwanawe Yazidi kwa aliyonayo na asiyokuwa nayo. Kisha akawaambia, 'Basi kwa hivi anastahiki kuwa Khalifa wa Waislamu…' " Imam Hussein a.s. akamjibu, Sheikh Abdalla anaendelea (uk. 26), kwa kumtajia "sifa mbovu za Yazid na akamwambia, 'Usizidishe madhambi kuliko uliyoyachuma. Yamekutosha hayo.' Na akamwambia, 'Unaudhulumu Uislamu na Waislamu kwa hayo uliyoazimia kufanya.'"

 

Baada ya kutofaulu mbinu zake hizo, aliamrisha waitwe mabwana wote watatu: Abdur Rahman bin Aby Bakr, Abdulla bin Umar, na Abdalla bin Zubeir. Sheikh Abdalla anasema (uk. 27), "Akawakaribisha wote pamoja kwa wakati mmoja. Akawaambia, 'Hili jambo la kufanywa Yazid kuwa Khalifa kishalichagua Mwenyezi Mungu na watu wote wameliridhia isipokuwa nyinyi. Basi tahadharini na kuleta balaa. Itakufikeni wenyewe kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu na yangu …' Wakampinga wote Akataka aseme faragha na Bwana Abdur Rahman bin Abi Bakr. Alipomwambia maneno hayo ya kutawalishwa Yazid, alimwambia, 'Hatutaki. Na ukiyapitisha kwa nguvu tutavirejesha upya vita vya mwanzo wa Uislamu; uwe na wenye shauri moja na wewe upande wa ukafiri kama alivyokuwa baba yako.' " Hapo Bwana Abdur Rahman akaondoka.

 

Baada ya siku tatu ikatoka amri ya kukusanyika watu wote wa Madina. Hapo Muawiya akawaweka wale wapinzani karibu yake, na akawaeleza waliohudhuria kuwa mikoa yote imemkubali Yazid kuwa Khalifa isipokuwa wao watu wa Madina, na kuwa lau yeye (Muawiya) angelikuwa anamjua aliye bora kuliko Yazid, angelimtawalisha; lakini hakuna bora kuliko yeye! Kisha akawaonya asisikie "kupinga kokote kule". Na akatangaza mkutano mwengine jioni.

 

Kabla ya huo mkutano, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 28 -- 29), aliweta wale wapinzani "wote pamoja ili atoke nao wende mkutanoni. Walipofika akawaambia: 'Nimekwisha weka machakari (wauaji) huko mkutanoni. Na mimi nitawaambia watu wote huko kuwa nyinyi nyote sasa mmekubali kutawalishwa Yazid. Asiyetaka roho yake ainuke hapo anipinge. Papo hapo kitaonekana kichwa chake kinagaragara chini.' " Na huko mkutanoni alikuwa ameshawaambia "mbele hao maaskari kuwa ye yote atakaesema kitu muuweni. Na akafanya ijulikane habari hii kwa watu wote ili wote wawemo katika khofu."

 

Haya! Huyo ndiye Muawiya! Na hivyo ndivyo  alivyopanga kumtawalisha mwanawe (Yazid) ambaye leo mawahabi wetu wasema kuwa mtu kama huyo ni Amiirul-mu'minin! Astaghfirullaah!

 

Inshallah, katika karatasi yetu ijayo, tutayaeleza yaliyotokea huko mkutanoni na aliyoyafanya Yazid baada ya kutawalishwa. Kisha tujiulize tena: mtu kama huyo kweli aweza akawa Amiirul mu'minin?

 

ABDILAHI NASSIR

S.L.P. 84603

MOMBASA

 

1 Safar, 1424

4 Aprili, 2003

 

(Inaendelea)