HOME

(3)

 

BARUA YA WAZI KWA MAWAHABI

 

Katika karatasi ya pili, kabla ya kuonyesha kuwa ni muhali Yazid kuwa Amiirul-mu'minin, tulianza kwa kueleza jinsi alivyoupata utawala wake. Kwa yaliyoandikwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy katika vitabu vyake tulivyovinukuu mpaka sasa hivi, inatudhihirikia kuwa aliupata kwa yeye kumuuwa Imam Hussein a.s., kwa babake (Muawiya) kuvunja ahadi aliyopanana na Imam Hassan a.s., na pia kwa kutumia hongo, vitisho na mabavu. Leo tuendelee na yaliyobakia.

 

Baada ya Imam Hassan a.s. kufa kwa ile sumu, Muawiya alipanga mikakati yake ya kumtawalisha mwanawe (Yazid). Lakini, hata hivyo, haikuwa rahisi. Anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 18 wa kitabu chake, Maisha ya Sayyidna Huseyn, ni kwamba "aliona ni uzito kabisa kutaka kulivunja jambo hili, sharti alichukulie mbinu kwa taratibu, akaona awafundishe Maliwali wake watoe fikira hii, isiwe imetokana na yeye. Akawaambia walisemeseme wenyewe tu huko katika nchi wanazoziendesha kama mchezo tu hivi kwanza."

 

Baada ya hapo, aliwakusanya wote mahali pamoja na, kama alivyowafundisha, ikawa mmoja baada ya mmoja husimama na kupendekeza utawala aachiwe Yazid. Lakini hata hivyo, si wote walimkubalia Muawiya; wengine walipinga: mmoja wao akiwa Al Ahnaf bin Qays. Huyu, Sheikh Abdalla S. Farsy anatwambia (uk. 20 wa hicho kitabu chake), alisema hivi: "La! Sisi watu wa Iraq sote si radhi kwa haya, na watu wa Hijaz wote pia hawawafiki. Hatumridhii kattu Yazid kuwa Khalifa wa Waislamu. Na wewe unamjua zaidi mwanao, kuliko watu wengine, kuwa hafai. Usijitwike mzigo wa kukutia Motoni kwa khiyari yako. Sisi haturidhii ila kizazi cha Ali.”

 

Mambo yakakorogeka. Sheikh A. S. Farsy anasema (uk. 20): "Akainuka Abu Khunayf akatoa upanga wake akamwonyeshaMuawiya akamwambiya 'Asiyekubali mlishe huu atashika adabu yake'. AkainukaMuawiya akasema, 'Huyu ndiye khatibu barabara. Khatibu vitendo si maneno tu. Na huyu ndiye bora wa wote waliohudhuria hapa na wengineo'. Baraza ikavunjika."

 

Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume s.a.w.w., aliposikia habari hiyo, Sheikh A. S. Farsy anaendelea (uk. 21), "alikasirika sana sana kuona vile … Muawiya anazivunja zile ahadi alizompa Sayyidnal Hasan…"

 

Mambo yakamalizikia hapo, yasende mbele zaidi. Lakini baada ya muda (mwaka wa 50 BH), Muawiya alikwenda Madina, asemavyo Sheikh A. S. Farsy (uk. 21), "kugonga gogo asikie vipi mlio wake". Huko alikutana na "watoto wa kisahaba wenye jina kubwa kabisa"; nao ni mabwana "Abdulla bin Abbas bin Abdul Muttalib (hakuweta ndugu zake), Abdulla bin Jaafar bin Abii Talib bin Abdil Muttalib (hakuweta ndugu zake), na Abdulla bin Zubeir bin Awam (hakuweta ndugu zake) wala hakumwita Sayyidnal Huseyn." Akasema nao kwa ulatifu ili wamkubali Yazid, lakini wote wakapinga; na baada ya siku mbili tatu, akenda zake mtungi mtupu!

 

"Alipokufa Sayyidnal Hasan", Sheikh A. S. Farsy anazidi kutueleza (uk. 22), "…Muawiya aliwaamrisha watu wa Sham wote wamkubali Yazid kuwa ndiye Khalifa baada yake. Wakakubali wote kwa umoja wao."  Akamwamrisha Liwali wa Madina awalazimishe watu wake nao wamkubali Yazid. Yeye, anavyosema Sheikh A. S. Farsy (uk. 23), "yakamuudhi haya akaona kwa nini tumkubali kijana asiyekuwa na mwendo mzuri atutawale sisi watu wazima na Masahaba". Kwa hivyo akamjulisha Muawiya msimamo wake, na Muawiya papo hapo "akamwandikia barua ya kumtoa katika Uliwali".

 

Alipopata barua hiyo, Liwali huyo (Marwan bin Hakam) alihamaki "sana sana na akachukua wakubwa wa jamaa zake wa kukeni  --  Bani Kinana  --  mpaka Sham kwa Muawiya kumtishia kuwa atafanya thora (mapinduzi). Muawiya akamwogopa akampa  --  na akawapa na hao jamaa zake  --  maneno mazuri na fedha nyingi na mshahara wa maisha. Yeye pouni mia tatu kila mwezi, na kila mmoja katika hao jamaa zake pouni khamsini kila mwezi."

 

Huko Madina, Liwali mpya aliifuata baraabara ile amri ya Muawiya ya kuwalazimisha watu wake wamkubali Yazid. Lakini hawakukubali; walipinga. Liwali akamjulisha Muawiya hilo pamoja na kumtajia waliokuwa mstari wa mbele katika upinzani huo. Naye akampelekea "barua za watu hao, akamwamrisha awapelekee na amletee jawabu ya kila mmoja katika wao. Nao ni mabwana hawa: Abdulla bin Abbas bin Abdil Muttalib, Huseyn bin Ali bin Aby Talib bin Abdil Muttalib, Abdalla bin Jaafar bin Aby Talib bin Abdil Muttalib, na Abdalla bin Zubeir bin Safiyya bint Abdil Muttalib."  Aliwaandikia  "maneno makali kabisa", Sheikh A. S. Farsy anaeleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho, "na kuwahadidi kuwa atawaua wakikataa kumkubali Yazid awe Khalifa baada yake."

 

Baada ya hapo ilikuaje? Hilo tutalizungumza katika karatasi ijayo inshallah. Kwa sasa tunauliza tena: Anayetawalishwa hivyo huweza kuitwa Amiirul-mu'minin? Ndivyo Kiislamu hivyo?

 

 

ABDILAHI NASSIR

S.L.P. 84603

MOMBASA

 

22 Muharram, 1424

26 Machi, 2003

 

(Inaendelea)