HOME

(2)

 

BARUA YA WAZI KWA MAWAHABI

 

Katika karatasi yetu ya kwanza, kinyume na walivyodai mawahabi katika karatasi yao, tulionyesha kwamba si "urongo", wala si uzushi wa mashia, kusema kuwa Imam Hussein (a.s) na watu wake waliuliwa kinyama kwa kukatwa vichwa vyao huko Karbalaa, Iraq. Tuliyatia nguvu maneno yetu hayo kwa ushahidi wa yaliyoandikwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy katika kitabu chake kiitwacho Maisha ya Sayyidna Huseyn. Leo inshallah tutalijadili dai lao jengine: la kuwa ati Yazid, ambaye chini ya utawala wake ndipo mauwaji hayo yalipofanywa, alikuwa "Amirul-muuminin"!

 

Lakini kabla ya kuonyesha kuwa mtu huyo  --  kwa vipimo vya Kiislamu  --  hakuwa, wala hawezi kuwa hivyo, ni muhimu kwanza tuelewe jinsi alivyoupata utawala wake huo. Na hilo, kama tulivyofanya katika karatasi yetu ya kwanza, tutamwachia Sheikh Abdalla S. Farsy alifanye japokuwa aliyoyaandika yeye, tukilinganisha na yaliyoandikwa na wanazuoni wengine wa kisunni kwa lugha ya Kiarabu, ameyazimua mno.

 

Kabla ya Yazid kutawala katika mwaka wa 60 BH, Waislamu walitawaliwa na babake aliyekuwa akiitwa Muawiya bin Abii Sufyan. Wote wawili hao  --  babake na babu yake  --  walisilimu kwa kukosa budi baada ya Makka kutekwa na (kabla ya hapo) baada ya kuongoza upinzani mkali dhidi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na kushindwa.

 

Huyo Muawiya ndiye yule aliyesimama kumpinga na kumpiga vita "Khalifa wa Nne" (Imam Alii bin Abii Twaalib a.s.) alipochaguliwa na Waislamu kuwa Khalifa wao; na baada ya Imam Alii (a.s) kuuliwa, akaingia kumpinga na kumpiga vita Imam Hassan a.s. (ndugu yake Imam Hussein a.s.) ambaye, anavyotwambia Sheikh Abdalla S. Farsy, aliuliwa "kwa sumu" na yeye huyo Yazid tunayeambiwa kuwa ati ni "Amirul-muuminin"! (Tizama uk. 24 wa kitabu chengine cha Sheikh Abdalla S. Farsy kiitwacho Maisha ya Sayyidna Hassan (chapa ya 1999) kilichochapishwa na Adam Traders wa Mombasa vile vile).

 

Lakini kwa kiasi cha miaka kumi kabla ya kupawa hiyo sumu, Imam Hassan (a.s) na Muawiya, babake Yazid, baada ya vita vikali, walifanyiana suluhu na kuandikiana mkataba. Kati ya waliyokubaliana katika mkataba huo, anavyotueleza tena Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 16 wa kitabu chake hicho, ni kwamba Imam Hassan (a.s) amwachie Muawiya Ukhalifa. Lakini Muawiya akifa, basi Imam Hassan (a.s) ataukamata yeye. Na lau Imam Hassan (a.s) atakufa, basi ushikwe na Imam Hussein (a.s).

 

Kuona hivyo, Sheikh Abdalla S. Farsy anaendelea kutueleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho hicho cha Maisha ya Sayyidna Hassan, "akili ilimjia (Yazid) akaona kuwa huu ufalme wa baba yangu utanipotea kwani akifa baba yangu atatawala Hasan, wala haikuandikwa kuwa akifa nitatawala mimi. Akaona amuue kwa sumu. Akapeleka watu madhubuti kwa siri kwa mke wa mwisho wa Sayyidnal Hasan, wala hakuzaa naye, akiitwa Jaada bint Ash-ath. Wamtumainishe kuwa akimuua huyu mumewe atamuoa Yazid na tangu sasa atampa dirham laki moja,, na mengineyo makubwa kabisa anayoyataka. Bibi akavutika akampa sumu kali kabisa huyo mumewe. Akasononeka muda wa siku arbaini; kisha akakata roho hali ya kuwa shahidi…"

 

Na katika uk. 18 wa Maisha ya Sayyidna Huseyn, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema: "Kabla ya kufa Sayyidna HasanMuawiya aliona ajifungue na ahadi ya kumtawalisha Al Hasan wala hana ahadi ya kumtawalisha mwengine. Basi aliona amfanye mwanawe anayempenda zaidi  -  naye ni Yazid  -  awe waliyyul ahdi (heir-apparent). Itangazwe kwa raia wote kuwa akifa yeye hakuna uchaguzi wowote ila kuwa mwanawe  -  Yazid  -  ndiye Khalifa tu. Akiridhia Hasan asidhie na mwengine yeyote yule akiridhia asiridhie." Akamalizia kwa:  "Maliwali wake wengine  --  kwa ajili ya kutaka kujipendekeza ili waendelee na Uliwali wao  --  walimtia nguvu katika fikira hii ijapokuwa siyo ya Uislamu…"

 

Inshallah tutaendelea na yaliyobakia, ya jinsi Yazid alivyotawalishwa, katika karatasi ijayo. Kwa sasa tunalopenda ujiulize, ewe ndugu msomaji, ni: Kweli, mtu anayetawalishwa kama ilivyoelezwa hapo juu, huwa ni "Amirul-muuminin"? Hivyo ndivyo Uislamu usemavyo?

 

ABDILAHI NASSIR

S.L.P. 84603

MOMBASA

 

15 Muharram, 1424

19 Machi, 2003

 

(Inaendelea)