rudi maktaba >Maadili >Yaliyomo >

SIFA ZA DINI

Mpaka sasa nimeeleza umuhimu wa dini kwa ujumla.

Sasa hebu ngoja nizitaje sifa za lazima kwa dini kuwa nazo, ili itimize mahitaji ya dini niliyoyataja hapo juu.

1) Kwanza kabisa dini ni lazima ipatane na akili na udadisi wa mtu.

Hakika zipo dini zenye kuwataka wafuasi wake waamini kwanza kisha ndipo waelewe. Kusema kweli dini kama hizi huzirudisha nyuma fikara za mwanaadamu na ni haki ziitwe (na kwa hakika zinaitwa) dini zisizopatana na fikara za Mwanaadamu.

Uislamu kama unavyofafanuliwa na imani ya madhehebu ya Shia Ithna-sheria, hutoa nafasi ya mbele zaidi kwa akili za binadamu na hoja zake. "Akili" ni moja wa misingi minne ya Sheria ya Shia Ithna-Asheria. Sio hivyo tu, bali vile vile imani hii inahimiza kuwa mafundisho ya dini ni lazima yaeleweke kwa mwenye kuiamini dini hiyo.

2) Ni lazima dini ifundishe na ifanye kwa vitendo, hekima ya mwanaadamu.

Ziko dini ambazo huwataka wafuasi wake wasujudie picha au sanamu za watu fulani fulani au wanyama fulani fulani au vitu vingine ambavyo havina uhai.

Dini kama hizi hushusha sana heshima za wafuasi wao, na ni haki zilaumiwe kwa jambo hilo. Baadi ya dini hufundisha ubora wa watu wa taifa fulani au kudharau watu wa ukoo mwingine.

Uislamu tu ndio uliokuwa na bado ni kiongozi wa usawa wa binaadamu na ambavyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya dini, umefundisha na ukafanya kwa vitendo, udugu, usawa na haki kwa binadamu na ukaonyesha heshima ya Mwanadamu kiasi cha kuweza hata kuyashangaza macho ya watu wote.

3) Dini ni lazima iwe mwongozo ulio kamili wa kumwendeleza mwanadamu kimwili, kiakili na kiroho kwa ujumla.

Zipo baadhi ya dini ambazo hutilia mkazo zaidi katika mambo ya kiroho na kuachilia mbali mwili na akili; na zipo nyingine ambazo huzungumzia tu kuhusu maendeleo ya kimwili, au ya kiakili lakini haziyafanyi kimatendo mambo hayo.

Dini za aina hii haziwezi kuwachukua wafuasi wake mbali sana kwa sababu maendeleo yafundishwayo na dini hizo yamekwenda kombo.

Ni Uislamu tu, kama unavyofundisha na Madhehebu ya Shia Ithnaasheria, ambao humwendeleza mtu kimwili, kifikara na kiroho kwa ujumla.

4) Ni lazima dini iwe na mkusanyiko wa sheria zihusuzo maisha ya binaadamu.

Dini ambazo hufundisha tu kuwa "wapende jirani yako" bila ya kuonyesha jinsi ya kufanya hivyo, ni dini zisizo na faida yo yote wakati zikaribiwapo na suala la kulifanya jambo kimatendo.

Uislamu unao mkusanyiko timamu wa sheria za maisha ya mwanaadamu ambazo humwongoza mtu sawa sawa katika maisha yake ya kifamilia, kijamii, kiuchumi, kitabia za kiutu na kiadilifu.

5) Ni lazima dini iafikiane na asili ya mwanaadamu.

Zipo dini zinazojaribu kuiepuka asili ya mwanaadamu. Kwa mfano, baadhi ya dini zinafundisha utawa. Wanaamua kwa matendo yao (kama si kwa maneno mengi) kuwa Mwenyezi Mungu alikosea alipoumba hamu ya tendo la mke na mume katika mwili wa mwanaadamu. Vile vile wanasahau (au wanajifanya kusahau) kuwa silika za kiasili haziwezi kuharibiwa na kuwa silika hizi zisizo za kiasili zinamwongoza mtu kwenye undanganyifu wa kisiri.

Na sijui, ni nini kingelitokea kuhusu kuwepo kwa mwanaadamu hapa duniani, iwapo watu wote wangelikuwa wafuasi wa kimatendo wa dini hiyo. Hakika watu wote wangelimalizika katika muda wa miaka kati ya arobaini na hamsini hivi.

Bila ya kusema kuwa dini kama hii haiwezi kuwaongoza watu kwenye ustawi, kwa sababu kufuatana na asili yake, dini hii ni kinyume na mdumisho wa kuwepo kwa wanadamu hapa duniani.

6) Ni lazima dini isitumike kama zana mikononi mwa wadhalimu, ili kuudhulumu umma.

Dini nyingi zinalaaniwa na makafiri kwa kuwa silaha ya makabaila kwa ajili ya kuudhulumu umma unaoonewa na kuzifunika sauti za walalamikaji.

Dini kama hizi, kwa mfano zile zilizofundisha mawazo ya "Kudra". Hivyo basi, umma ulilazimishwa kuamini kuwa matendo yote mabaya, udhalimu, na uovu wa watawala ulikuwa ni Penzi la Mwenyezi Mungu; hivyo basi vitu kama hivi ni lazima vivumiliwe bila ya malalamiko yo yote.

Dini kama hizo hazina nafasi katika karne iliyoendelea kama hii yetu. Ni Uislamu peke yake, kama ulivyoelezwa na madhehebu ya Shia Ithna-asheria ambao ulisema kuwa imani kama hiyo ilikuwa upuuzi mtupu; kuwa kila mtu ana madaraka kamili ya matendo yake na kuwa madaraka yake yasihusishwe na Mwenyezi Mungu.

Itadhihirika wazi, kutokana na kanuni ya hapo juu kuwa, miongoni mwa dini nyingi sana za duniani, ni Uislamu tu (Imani ya Shia Ithna-asheria) ambao Unatimiza mashaiti haya ya lazima ya dini ya kweli, na yenye maarifa mengi.