rudi maktaba >Akida >Yaliyomo >

FAIDA ZA DINI NI ZIPI?

Zipo sababu nyingi zimfanyazo mwanadamu ahitaji Dini.

(1) Sote twajua kuwa mwanadamu ni mnyama ahitajiye kuishi kijamii pamoja na wenzake. Kila mtu anategemea mamilioni ya watu wenzake kwa maisha yake na kwa mahitaji muhimu ya hayo maisha yake. Pia tunajua kuwa kila jamii inahitaji sheria fulani fulani ili kuzuia dhulma na kuhifadhi haki ya kila mtu katika jamii hiyo. Lakini basi swali lifuatalo ni hili, ni nani aliye na haki ya kutunga Sheria hizo? Mtu mmoja? (mtu huyo na awe mfalme au mtawala wa Kiimla)! Jibu ni "Hapana." Yeye hataweza, maana kwa ajili ya silika za kibinadamu, atatunga sheria kwa kufuatana na tamaa yake ya kibinafsi.

Kikundi cha watu? (Watu hao na wawe wa kikundi cha Utawala wa watu wa koo Bora au wa kikundi cha kidemokrasi)! Jibu ni kuwa, "Hawa pia hawataweza kuifanya kazi hiyo vipasikavyo, maana kila mmoja wao hawezi kujiepusha na uamuzi usio sawa na wingi wa uamuzi usio, sawa, hauwezi kupatana na uamuzi ulio sawa.

(2) Vile vile ni dhahiri kuwa hakuna kikundi cha watu kiwezacho kujiepusha na kujitia katika tamaa za kibinafsi. Kwa mfano katika siku za utawala wa kikoloni, mabunge na halmashauri za Makoloni zilikuwa zikitunga sheria kufuatana na mapendekezo ya watawala wa Kizungu. Siku hizi, mabunge na Halmashauri hizo hizo hutunga sheria kufuatana na mapendekezo ya wananchi. Kujali ubinafsi kulikuwa na bado kungali jambo muhimu la kutunga sheria duniani pote.

(3) Zaidi ya hapo hakuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kutunga sheria za mambo mengi na ambazo zimo katika msingi wa usawa na uadilifu kamili.

Kwa sababu hiyo, ni lazima sheria hizo zitungwe na mtu fulani ambae ni mbora kuliko mwanadamu, ambae hana chochote cha kupoteza au cha kufaidika nacho kutokana na sheria hizo, na ambae kila mwanadamu ana uhusiano wa aina iliyo sawa kwake.

NA "MTU HUYU" NI ALLAH. Kwa sababu hiyo tunawajibikiwa kuwa na dini.

(4) Zaidi ya hapo ni kuwa, sheria na desturi zilizotungwa na mwanadamu zina upungufu mmoja mbaya sana: Sheria na desturi hizo haziwezi kuzuia matendo ya jinai. Upungufu huu, hukufanya kuwepo kwa sheria za aina hii kuwa kusiko na faida yo yote.

Kwa mfano, mwizi anaingia nyumba isio na watu, katika kijiji cha ughaibuni, usiku wa manane kwa ajili ya kutaka kuiba vitu vyenye thamani. Yeye aelewa wazi kuwa hakuna mtu aiwakilishaye Serikali, kwa maili nyingi sana kutoka nyumba hiyo. Hivyo ataona kuwa na usalama kutokana na kukamatwa. Je! Katika hali hii, iko sheira ya serikali ambayo itamzuia mwizi huyu kutimiza jinai hii? Jibu ni kuwa "HAKUNA".

Kusema kweli hakuna serikali itakayomzuia mtu huyu asiibe lakini Dini inaweza, Dini iliyo ya kweli, kama tulivyoieleza hapo juu, huwafundisha watu kuwa yupo Mwenyezi Mungu, ambae ajua kila kitu na anayeona kila kitu. Yeye Mwenyewe ni Mwadilifu na Mwema na anatutaka nasi tuwe waadilifu na wema; kuwa tunahusikana na matendo yetu mbele yake na tutakuja mpa hesabu ya matendo yetu baada ya kufa kwetu.

Kama mtu anaiamini dini hiyo basi, hivyo (Na kwa hivyo tu) anaweza kujiepusha na kutenda dhambi, majinai na kuwadhulumu watu wengine popote awapo.

Sheria za serikali zaweza kuzuia mtu kutenda matendo mabaya ya wazi wazi na hata hivyo, ni katika muda na mahali ambapo mikono ya serikali hiyo yaweza kupafika. Lakini kumwamini Mwenyezi Mungu na dini, hutawala si matendo ya mwanadamu, ya kiwazi wazi tu bali hata yale yaiiyojificha na yaliyo mawazo ya moyoni pia.

Utawala huu, hauna mipaka kwa kutegemea mahali maalum au muda fulani, kwa sababu Mwenyezi Mungu yupo kila mahali na anaona kila kitu.

(5) Ili kuzielewa vizuri faida zilizo wazi wazi, ambazo jamii yazipata kutokana na imani ya kuwepo Mwenyezi Mungu na dini, hebu jaribu kufikiria machafuko na ghasia ambazo wanaadamu wangeliweza kujitia, kama imani ya kuwepo Mungu ingalitupiliwa mbali. Hakutakuwa na jamii yoyote. Badala yake, kutakuwa na umati wa watu tu. Katika hali hiyo, kila mmoja anao uhuru wa kufanay chochote kile akipendacho. Mtu atafikia kuwa hakuna Mungu, na hakuna maisha ya Akhera, na kuwa yeye amekuwepo hapa duniani kwa bahati ya hali ya asili iliyojitokeza tu. Na pia anajua kuwa muda wa maisha ni mfupi. Kwa hivyo, kikawaida atashawishika na kuyafaidi maisha kwa kadri iwezekanavyo bila ya kujali kitu chochote kile. Kitu atakacho kiwazia ni kujaribu kuepeka kukamatwa akiwa anatenda jambo lolote baya, au kuonwa na serikali tu. Na wakati wowote atakaojiona kuwa yu salama, hataacha kutenda jinai lolote ili kujikidhia tamaa zake, bila ya kujali dhara la tamaa yake hiyo kwa wenzake.

Swali: Hata MIahidi (mtu asiyeamini kuwa kuna Mungu) anaweza kuishi maisha mema kama yale ya mfuasi wa dini. Kama jambo hili lawezekana bila ya dini, nini basi faida ya dini?

Jawabu: Ni kosa kufikiria kuwa, maisha mema ya mlahidi hayana uhusiano kabisa na dini; kwa sababu fikara hizo njema hazikuhifadhiwa akilini mwa mtu huyo na kitu kingine chochote ila na dini tu. Mafundisho mema ya kidini yameimarishwa akilini mwa mtu kwa maelfu ya miaka. Yamekuwa yakihifadhiwa toka kwa baba hadi kwa mwana kwa njia ya asili ya mwanadamu ya mwana kurithi tabia za baba; na pia toka rafiki hadi rafiki kwa njia ya mazingira. Hizi faida njema zimekuwa zisizotengeka toka akilini mwa mtu huyo.

Lakini, akili ni nini? Akili ni fikara za kidini na kiutu ambazo zimemwingia mtu huyo kutoka kwa Wahenga wake wenye maisha ya kidini; na ambazo yeye hawezi kuziepuka. Akili inategemea na mafunzo mema ya dini.

Je ni kwa muda gani akili yaweza kubakia kichwani mwa mtu wakati mafundisho ya kidini yaondolewapo kabisa toka kichwani mwa mtu huyo?

Jibu ni kuwa: Mtu ye yote yule alifikiriaye jambo hili kwa makini ataamua kuwa, hakuna vime unaweza kubakia mwilini mwa mtu, kama utatengwa na imani ya kuwepo Mungu na dini.