rudi maktaba >Akida >Yaliyomo >

DINI NI NINI?

Neno hili lenye asili ya Kiarabu, "Diin (dini) linatumika kwa maana nyingi kidogo.

(1) "Uislamu; imani ya Umoja wa Mwenyezi Mungu; Ibada; Utii; Matendo yote ya kiibada na Ucha Mungu." Maana zote hizi zinahusiana zenyewe kwa zenyewe na zahusika na imani ya kuwepo Muumba.

(2) "Hukumu; Thawabu au Adhabu; Hesabu Amri; Sheira."

Maana hizi, nazo pia, zahusiana zenyewe kwa zenyewe na zatushabihisha kwenye imani ya Maisha ya Akhera.

(3) Kikundi cha tatu cha maana ya neno hili ni "Desturi; Tabia; Mazoea; Aina zote mbili za Dini iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu au ya kimapokeo kutokana na wahenga."

Maana hasa ya neno hili Diin ni kuwa mwanadamu kwa silika zake za asili, hana budi kuwa na mpango wa maisha wenye msingi wa fikara za kiroho au fikara zile tuziitazo "Imani".

Hivyo basi, inaonekana kuwa, neno "ad-Diin" lina maana kubwa mno kuliko ile ya neno la Kiingereza "Religion", ambayo husisitiza maana ya Mwanadamu kuitambua Nguvu kubwa kuliko yeye, na ambayo inautawala ulimwengu mzima, na hasa Mungu au miungu ya mtu kibinafsi, ipasikayo kutiiwa na kuabudiwa; matokeo ya utambuzi wa aina hiyo; mwongozo wa kiroho wa mtu; au mpango maalum wa Kiimani na kiibada.