rudi maktaba >Akida >Yaliyomo >

IMANI HALISI YA KUMUAMINI NA KUMPWEKESHA MWENYEZI MUNGU MMOJA IMEHUISHWA

"Kwa hiyo nawaambieni, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, na litapewa taifa jingine lenye kuzaa matunda". (Mathayo 21:43)

Wafuasi wa Yesu walifurahia sana maelezo haya wakiamini kuwa wao ni "Watu wateule" wapya wa Mungu. Hata hivyo, ukristo unaendelea kupotea kutoka katika njia iliyonyooka.

Mpaka kufikia karne ya nne, ukristo ulikuwa umejiimarisha vizuri kama dini, imani na misingi yake ilipangwa vizuri hasa kwa vile ulikuwa ndio Hukumu na mwongozo wa Maandiko kwa wafuasi wake.

Kama tulivyoona hapo awali, mafundisho sahihi ya Yesu yalikuwa yamesahauliwa na badala yake yakafuatwa mafundisho ya Paulo wa Tarsus. Imani na mila za kipagani ziliingizwa katika Ukristo, na Paulo ili apate wafuasi miongoni mwa Watu wa mataifa (Gentiles) waliokuwa wapagani wa zama zake, imani na misingi yote ya Kikristo imetokana na upagani (ukafiri). Kwa kadri wapagani walivyokuwa wakiingia katika Ukristo kwa wingi zaidi, ndivyo imani zaidi za kipagani zilivyokuwa zikiingia zaidi katika Ukristo.

Sikukuu zote za kikafiri (kipagani) zilihamishiwa katika Ukristo: Siku ya kuzaliwa mungu wa wapagani (sanamu) aliyeitwa Mithras ambayo ilikuwa tarehe 25 Desemba (mwezi wa 12). Alifanywa kuwa ndiyo siku ya kuzaliwa Yesu ambapo pia vitendo vya ibada hii ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu vilichukuliwa kutoka kwenye vitendo vya sherehe za Warumi za kusherehekea kuzaliwa Saturn. Sherehe hizi zilifahamika kwa jina na Saturnalia. Sikukuu ya wafu (wa kipagani) ilifanywa kuwa ni siku ya watakatifu wote; siku iliyotengwa kwa ajili ya kusherehekea kufufuka kwa mungu wa kisanamu aliyeitwa Attis, ilifanywa kuwa ndio siku ya kufufuka kwa Yesu, ambayo pia vitendo vingi vya sherehe hii vilichukuliwa pia kutoka kwenye upagani kwa madhumuni yale yale.

Sabato ya Wayahudi, iliyopangwa na Mungu kuwa iwe siku ya saba ya wiki katika sheria ya Musa, ilibadilishwa na Ukristo na kufanywa kuwa ni siku ya kwanza (yaani badala ya Jumamosi kuwa siku ya saba ilifanywa kuwa ni siku ya kwanza). Jumapili ikajadiliwa kuwa ifanywe kuwa ndio siku aliyofufuka Yesu, lakini lazima ikumbukwe kwamba Jumapili ilikuwa ni siku ambayo Mungu wa kisanamu, Mithras, "aliliteka jua".

Dhana ya ukristo juu ya masuala ya ngono (sexuality) na ndoa iliathiriwa sana na mila za kipagani zilizokuwa katika dini na falsafa za kipagani za "Neoplatonism", Stoicism na Gnosticism (utawa). Dini zote hizi ziliamini kuwa kujamiiana (ngono) hata ndani ya ndoa ni jambo ovu sana, na kwamba kutooa na kutoelewa ni sifa kubwa na nzuri sana ambazo kila mtu inambidi ajitahidi kuzipata. Ukristo kwa moyo mkunjufu uliyachukua mawazo haya na hivyo kumuweka mwanadamu na familia kwa ujumla katika hali isiyokuwa asili yake na ambayo ni tofauti na maumbile yake na ambayo kamwe Mungu hakuamrisha hivyo.

Vitendo vya ibada na imani za kipagani zilizoingizwa katika ukristo zilikuwa zinawakera na kuwapa taklifu kubwa wamishenari wa kikristo wa mwanzo, hasa kwa vile mila na tamaduni hizi zilikuwa zimeimarika mno ambapo kwamba ilikuwa haiwezekani kuziondoa kwa namna yoyote ile. Katika mwaka 598 B.K., Papa Gregory, the Great, aliwasaidia mapadri kwa kuwaambia kwamba wanatakiwa kuwaruhusu watu kufuata mila na imani zao za zamani, isipokuwa tu hili linatakiwa "likusudiwe" katika "kumsifu" Mungu. Kwa hiyo watu waliendelea na imani zao katika uchawi, kurogana, mizuka, n.k. kwa vile mapadri waliwaambia kuwa udanganyifu huu ulikuwa ni "kudhihirika" kwa shetani. Watakatifu na "warithi wa watakatifu" walihimizwa zaidi, kwa vile wao waliaminiwa kuwa na nguvu za kumfukuza shetani.

Ukristo, ukiwa umeelemewa na idadi kubwa ya imani na desturi za kikafiri (kipagani) pamoja na kumtambua Yesu -- badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ndio kiini cha imani yao; ulikuwa umebakia kuwa ni uchafu tu usiokuwa na lolote isipokuwa uchafu.

Haja ya Mtume Mwingine

Wayahudi walipotelea katika vitabu vyao vya sheria; Wakristo walipotea kutokana na kumfanya kwao Yesu kuwa ni Mungu. Mwenyezi Mungu aliamua kumpa mwanadamu nafasi moja ya mwisho ili kuirejesha na kuihuisha imani halisi ya kumuamini na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mmoja tu asiyekuwa na mshirika.

Nabii Ibrahim, kama ilivyodokezwa katika sura ya kwanza alikuwa na watoto wawili wa kiume Is-haq na Ismail ambaye ndiye aliyekuwa mkubwa kwa Is-haq. Mungu alipoweka agano lake na Ibrahim kuhusiana na Is-haq, alikuwa pia na maneno kidogo ya kuzungumzia juu ya Ismail:

"Na kuhusiana na Ismail, Nimekusikia: Tazama Nimembariki, (nitamzidisha) nitauzidisha uzao wake; atazaa Maseyyid kumi na wawili (Maimamu kumi na mbili ) na Nitamfanya kuwa taifa kubwa". (Mwanzo 17:20).

Agano Lililofanywa kwa Ismail Limetimia

Ismail na mama yake walikaa Uarabuni ambapo waliishi na kuendelea, kwa kadri miaka ilivyokwenda, ndivyo walivyozidi kuwa taifa kubwa lililokuwa limebashiriwa na Mwenyezi Mungu. Katika mwaka 610 B.K. ahadi ya Mungu ya kukibariki kizazi chake (Ismail) ilitimia, wakati mmoja wa kizazi chake, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 40 aliyeitwa Muhammad (SAWW) alipoitwa na Mwenyezi Mungu ili kuleta ujumbe wake kwa wanaadamu wote.

Agano ambalo Mungu aliweka na Ibrahim sasa lilikuwa limekamilika, na uimarishaji wa imani halisi ya kumuamini na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mmoja asiyekuwa na mshirika (pure monotheism) -- Uislamu, au kujisalimisha na kujinyenyekesha kwa Mwenyezi Mungu Mmoja -- ulikuwa katika njia yake ya kubadilika kutoka kwenye ndoto kuwa kweli.

Kwa hakika baraka alizopewa Ismail zilikuwa kubwa kabisa kwani Mtume Muhammad alishuhudia katika kipindi cha maisha yake Uislamu thabiti kabisa ukisimama na kuimarika, na aliuleta ujumbe wa Mwenyezi Mungu katika mfumo ambao umeuwezesha kubakia bila kuharibiwa wala kubadilishwa hadi leo hii.

Misingi ya Uislamu ni misingi ya kuaminika na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mmoja asiyekuwa na mshirika: Ibada ya Mwenyezi Mungu na Mungu peke yake, na utii wa sheria yake. Kwa mara nyingine imani ya kumuamini na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mmoja ilirejeshwa na kuimarishwa.