rudi maktaba >Akida >Yaliyomo >

AGANO LILILOVUNJIKA

Akiwa amechoshwa na ibada ya masanamu miongoni mwa watu wake, Nabii Ibrahim aliiacha nchi yake karibu miaka 2000 kabla ya Yesu ili apate uhuru wa kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja.

Ilikuwa vigumu kwake kuicha nyuma familia yake. Hivyo Mwenyezi Mungu alimbariki kwa kumpa watoto wawili wa kiume. Kisha akamfariji Nabii Ibrahim kwa kumwambia kuwa mtoto wake mdogo, Is-haq atafanya naye Agano la Milele. Is-haq akazaliwa katika nchi ya Kiyahudi ya watu "Wateule" wa Mungu. (Baadaye tunaona ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa mtoto mwingine wa Nabii Ibrahim, Ismail).

Licha ya heshima na utukufu huu wa kuitwa "watu wateule" wa Mungu, Wayahudi waliendelea bila kuacha kurudia ibada ya masanamu na Mwenyezi Mungu aliendelea kupeleka Mitume mmoja baada ya mwingine ili kuwaonya Wayahudi juu ya kutoridhishwa Kwake na tabia yao. Baada ya maonyo kushindwa kuibadilisha tabia yao, nchi jirani zilizokuwa maadui ziliingia na kuwapiga vibaya Wayahudi.

Ingawa Mwenyezi Mungu aliwakubalia muda wa amani na nafuu mara nyingi aliposikia kilio chao cha kutaka rehema yake, lakini sasa hivi, hasira Yake ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba mnamo mwaka 581 kabla kuja Yesu, kwa sababu ya kiburi na jeuri yao iliyoendelea, Aliruhusu Wababiloni kuwafagia Wayahudi wote wa Ufalme wa Yuda Kusini, ambako Mfalme Nebuchadnezzar na jeshi lake waliosonga mbele na kuupiga vibaya mji wa Jerusalem na wakawachukua Wayahudi kama mateka.

Upande wa Juu wa Ufalme wa Kiyahudi wa Israel ulipatwa na balaa kama hili mwaka 721 kabla ya Yesu katika mikono ya Waassyria.

Wakiwa wametawanywa na jumba lao la ibada kuharibiwa vibaya, Wayahudi waliamua kuanza kufuata sheria ya Mwenyezi Mungu. Hata hivyo imani ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu mmoja asiye na mshirika ilikuwa imepotea kabisa, badala yake kulikuwa mvurugiko uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku wa mambo waliyoyaongeza wenyewe na mengine kuyapunguza katika vitendo vyao vya ibada.

Hivi ndivyo hali ilivyokuwa ulimwenguni katika kipindi ambacho Yesu alipokea wito kutoka Mwenyezi Mungu wa kumtaka aje kama Mtume kwa Wayahudi.