rudi maktaba >Akida >Yaliyomo >

Uchunguzi Makini Juu ya Ukristo

Tafsiri ya kitabu kiitwacho : A Closer Look at Christianity

Kimeandikwa na : Barbara Brown

Kimetafsiriwa na : Aziz Hamza Njozi

DIBAJI

Wengi wetu tunaridhika kuishi tu bila udadisi na tunayakubali mambo "kama yalivyo"; tunayapuuza na kuyadharau maswali madogo madogo yanayohitaji kujibiwa na yanayoleta mashaka katika akili zetu, hasa masuala yanayohusiana na dini. Kwa kufanya hivi, ndiyo ni kweli kwamba tunayopuuza, lakini kamwe hatupati utulivu wa akili na amani ndani ya nafsi zetu, kwa sababu daima nafsi zetu zinataka kuujua ukweli na sio kuupuuzia.

Wengine miongoni mwetu, hata hivyo, haturidhiki kuyachukua mambo kama yalivyo na hivyo kwa bidii na shauku tunafanya jitihada kuyatafutia majibu sahihi maswali yanayojitokeza katika maisha yetu. Tunahoji imani za baba zetu, hatupo tayari kuzikubali na kuzifuata kibubusa bila hoja na dalili za kutosha. Barabara hii haipitiki kwa urahisi kwa namna yoyote, lakini kwa mwenye bidii ya kutosha, malipo yake ni kuona ukweli, yakini, na utulivu wa akili.

Nimelelewa katika familia ya kikristo na nikakua katika madhehebu ya kiprotestanti yakieleweka kama "Imani ya kikristo iliyofanyiwa marekebisho." Licha ya ufuasi wangu mzuri wa dini - uhudumu wa kanisa mara mbili kila Jumapili na siku za mapumziko, darasa la (mafunzo ya) Jumapili, madarasa juu ya mafunzo, misingi na imani ya kanisa, shule za Biblia katika msimu wa kiangazi na kambi maalum juu ya Biblia - bado nilijikuta na maswali mengi kuhusiana na misingi halisi ya imani ambayo hakuna yeyote wala taasisi yoyote ya kidini ambayo ingeweza kuyajibu. Kwa miaka thelathini na saba nilitangatanga ndani ya ukungu wa utata kuhusiana na Mwenyezi Mungu na njia na namna sahihi ya kutoa heshima na utii wangu kwake mpaka mwaka 1991, nilipoupata Uislamu.

Mgogoro wa "Kimbunga cha Jangwani" katika Mashariki ya kati ulikuwa umefikia kilele chake, ubavuni mwa vitabu juu ya mbinu na silaha za kivita katika duka la vitabu mjini petu kulikuwa kitabu kidogo kilichoandikwa juu yake "Understanding Islam" (Kuuelewa Uislamu). Nilikifunua, nikiwa na hamu ya kutaka kujua juu ya dini hii "ya ajabu" ya Mashariki ya kati kama wenzangu wengi walivyokuwa wakitaka kujua juu ya dini hili. Udadisi wangu ghafla ulibadilika na kuwa mshangao, baada ya kusoma kurasa za kitabu hiki, nilikuta Uislamu umetoa majibu kwa maswali yangu yaliyokuwa yakinitatiza kwa miaka yote hii - sikupoteza muda zaidi, nikawa Muislamu. Baada ya muda mrefu sasa nikawa nimefikia na kupata nilichokuwa nikikitaka, kupata utulivu katika nafsi yangu juu ya uhusiano wangu na Mwenyezi Mungu.

Maadam Mwenyezi Mungu amenipa uwezo wa kujieleza vizuri katika karatasi, ninataka kuwafikia wale wote wenye maswali yanayowasumbua katika akili zao kuhusiana na dini, na nina matumaini kuwa huenda nikawasaidia kufikia majibu ya maswali hayo. Maelezo nitakayoyaeleza katika kitabu hiki yanaweza kuwashangaza na hata kuwashtua baadhi ya wasomaji, lakini kazi ya kutafuta ukweli daima huwa sio rahisi, hususan mbele ya imani zilizoaminiwa kwa muda mrefu na kanuni zake.

Nilianza kazi yangu siku nyingi kidogo kwa kuandika vijitabu vingi vidogo vidogo:

1) Tatu katika moja (three in one) uchambuzi wa imani ya Kikristo juu ya Utatu Mtakatifu kilichotolewa mwanzoni mwa 1993 na Shule Huria ya Chicago (The Open School of Chicago).

2) Kijitabu kiitwacho "A Closer Look at Christianity" (Uchunguzi makini juu ya ukristo) ambacho kinahusiana na uchunguzi juu ya ukristo kwa mujibu wa Biblia.

3) Kitabu kiitwacho "A Case of Corruption" (Suala la Maovu) ambacho kinahusiana na uongezaji na upunguzaji wa baadhi ya mambo katika Biblia.

Kitabu ulichonacho mikononi ni mkusanyiko wa vitabu vyote hapo juu, pamoja na utafiti zaidi nilioendelea kuufanya katika vitabu vyangu vya awali na vile vya mwisho kwa ajili ya wasomaji binafsi. Ni matarajio yangu kwamba, katika kurasa zinazofuatia, wasomaji watakuwa na nafasi ya kuona na kuelewa mtazamo wa ukristo kama mimi nilivyouelewa.