rudi maktaba >Maadili >Yaliyomo >

(8)

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Kama tulivyoahidi wiki iliyopita, leo tunaanza kuwajibu Ahlu-Tawheed kwa waliyoyaandika katika makaratasi yao waliyoyapa jina la "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulidi".

Katika makaratasi yao hayo, ndugu zetu hao wamenukuu baadhi ya maneno yaliyomo katika Barzanji na Burdah (vitabu viwili vinavyoeleza sifa za Mtume Muhammad s.a.w.w.) na kujaribu, kadri ya ujuzi na uweza wao, kuonyesha kwamba kusema maneno hayo ni shirki. Lakini, kabla ya kutoa majibu yetu, tuanze kwa kuyanukuu maneno yenyewe. Nayo ni mane yaliyotolewa katika Barzanji, na mawili katika Burdah.

Katika Barzanji wameyatoa yanayofuata:

"Na kama si yeye (Mtume s.a.w.) asingekuwa Alkhalilu (Ibrahim) na Adam. Na Musa (asingekuwepo) na Issa, bali hata Mulku Suleimani (usingekuwepo)."

"Ilisemekana alipotaka Mwenyezi Mungu, Mwenye Ezzi na Alietukuka, kumdhihirisha Mbora wa viumbe vyake, Muhammad, Rehma na Amani za Mwenyezi Mungu zimfikie. Akamuamrisha Jibril achukue Udongo wake (wa kumuumbia nao) kwenye mahali pa kaburi lake karimu".

"Alikuwa Mtume akikua mchana mmoja kama anavyokua mtoto mwengine kwa mwezi mzima kwa ajili ya kushughulikiwa na Mwenyezi Mungu".

"Akamwonyesha kwa haya macho ya kichwani (ya usoni) aliyomwonyesha. Nayo ni yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu."

Na katika Burdah wameyatoa yanayofuata:

"Kama si yeye (Mtume s.a.w.w.) usingetoka ulimwengu (usingeumbwa)."

"Haukupata kunipiga vita Ulimwengu, nikataka nusra kwa Mtume, ila huipata tu."

Hayo ndiyo maneno waliyoyanukuu ndugu zetu wa Ahlu-Tawheed kuthubutisha kwamba, katika vitabu hivyo, muna shirki. Wakayaandamiza, pia, na hujja zao za kuyabatilisha hayo.

MAJIBU YETU : Kwanza; tukumbuke kwamba tunalojadiliana si kuwa, katika vitabu vya maulidi, muna shirki au hamuna; la! Tunalojadiliana ni: maulidi ni bid'a au si bid'a; ni haramu au si haramu? Sisi, kwa upande wetu, katika makala yetu sabaa yaliyopita, kwa kujibu hujja zinazotolewa na wapinga maulidi, tumeonyesha kwamba maulidi si bid'a wala si haramu. Kwa hivyo sasa tunalolingojea kwa wapinga maulidi, wakiwamo Ahlu-Tawheed, ni majibu yao ya hujja tulizozitoa -- kiilimu na kimantiki, kama tulivyofanya sisi.

Pili; hata kama itakubaliwa kuwa hayo maneno waliyoyanukuu ni shirki -- na hilo hatulikubali kwa hujja tunayoitoa hapa chini -- hilo haliwi ni hujja ya kuharamishia maulidi au kuyasusia. La sawa kufanywa hapo ni kuyatoa hayo yanayoonekana ni shirki na / au kuyasahihisha; si kuzuia watu kuyasoma. Hivyo, kwa mfano, ndivyo alivyofanya marehemu Sheikh Abdulla Swaleh Farsy katika Wasila wa Nabahani. Yeye alipoona kwamba "Lawlaahu maa kunnaa walaa baaqiina" si sawa, hakuzuia watu, wala yeye hakuacha kuusoma. Alichofanya ni kukibadilisha kipande hicho na kukisoma alivyoona yeye ni sawa: "Lawlal ilaahu…" Hakuutupa wasila wote, wala hakuzuia watu kuusoma kwa sababu tu muna kipande cha maneno asiyoyakubali.

Tatu; tunapoyataamali yote madondoo sita waliyoyanukuu Ahlu-Tawheed, ambayo nasi tumeyanukuu hapo juu, hakuna hata moja liwezalo kusemwa ni shirki kwa hujja ifuatayo:

Shirki ni kusema / kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ana mwenziwe, au ana aliye sawa naye, au ana mfanowe, au ana anayetokana naye. Pia kusema / kuamini kuwa yuko muumbaji mwengine wa ulimwengu asiyekuwa Yeye, au muendeshaji (mudabbir) ulimwengu asiyekuwa Yeye, au mwenye haki ya kuweka sharia asiyekuwa Yeye, au anayelazimika kutwiiwa asiyekuwa Yeye, au kuna mtawala (haakim) asiyekuwa Yeye, au kuna mwenye haki ya kuabudiwa asiyekuwa Yeye.

Kwa kuwa hakuna hata moja, ya madondoo sita waliyoyanukuu Ahlu-Tawheed kutoka katika Barzanji na Burdah, linalosema hivyo, vipi basi mutakuwa muna shirki? Kama lipo, tunaomba watwambie ni dondoo lipi kati ya hayo waliyotutajia, na linaingia wapi katika hiyo taarifa ya shirki tuliyoieleza sisi hapo juu. Kama taarifa yetu imeacha mengine yaliyo shirki, basi tunaomba tukumbushwe.

Kwa hakika haikuwa nia yangu kuingia katika masiala ya shirki kwa sababu hilo li nje ya maudhui yetu. Maudhui yetu ni maulidi ni bid'a au si bid'a; ni haramu au si haramu. Na hilo tushalijibu vya kutosha. Lakini, kwa kuwa wafuasi wa madhihabi ya wapinga maulidi hupenda kukibandika jina la bid'a au shirki kila wanachokipinga wao, nimeona japo kwa ufupi niwaeleze wasomaji wangu jamaa zetu hao hupotelea wapi katika kuielewa shirki ni nini, na si nini!

Hilo, inshallah, tutalishughulikia wiki ijayo, kabla ya kuwajibu "Wakereketwa wa sunna Malindi".