rudi maktaba >Maadili >Yaliyomo >

(7)

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Wiki iliyopita tulidondoa baadhi ya mambo yanayofanywa maulidini ambayo, ama Qur'ani na / au Hadithi zimeyaamrisha, au zimeyapendekeza. Leo tunaendelea na yaliyobaki:

  • Kutoleana waadhi: Katika Qur'ani Tukufu (Sura 16:125) Mwenyezi Mungu anatuamrisha tulinganiane kwa hikima na mawaidha mema. Na vivyo hivyo ndivyo Bwana Mtume (s.a.w.w.) anavyotuhimiza katika Hadithi zake nyingi.
  • Jee, maulidini hatutoleani mawaidha na kulinganiana mema? Hayo nayo kama ni bid'a, sunna ni ipi?

  • Kumpenda Mtume (s.a.w.w.): Hadithi zake (s.a.w.w.) zatuhimiza tumpende, bali zinatueleza waziwazi kwamba hatuwi ni waumini mpaka tumpende yeye kuliko nafsi zetu, kuliko mali yetu na ahli zetu, bali kuliko watu wote.
  • Jee sifa zote zile anazosifiwa Mtume (s.a.w.w.) maulidini, furaha zote na nderemo zinazoonyeshwa maulidini, haziwi ni ushahidi wa mapenzi yetu kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.)? Mambo kama hayo hufanyiwa asiyependwa?

    Kama kuonyesha mapenzi yetu kwa Mtume wetu ni bid'a, sunna ni ipi?

  • Kujumuika na kushikamana: Qur'ani Tukufu (Sura 3:103) inatuhimiza tushikamane na tusifarikiane. Na Mtume naye (s.a.w.w.) anatuhakikishia, katika Hadithi zake, kwamba popote ambapo tutajumuika kwa kheri -- na sidhani kuwa maulidi ni shari -- basi Malaika watatuzunguka, rehema za Mwenyezi Mungu zitufinike, na utulivu wa nyoyo utushukie.
  • Jee, tunapokusanyika maulidini, hatuyaoni hayo? Ule umoja na mshikamano unaopatikana maulidini, wa wafuasi wa madhihabi mbalimbali kusahau hitilafu zao na kuwa kitu kimoja, ni rehema ndogo?

  • Kutembeleana na kukirimiana: Bwana Mtume (s.a.w.w.), katika Hadithi zake, ametunasihi tuwe tukifanyiana hayo; na hayo huyapata kwa ukubwa siku za maulidi. Waislamu wa mtaa mmoja, au mji mmoja, au hata nchi moja -- kwa kuhudhuria sherehe za maulidi ya wenzi wao -- hupata fursa ya kutembeleana na kukirimiana. Kwa njia hii hujuana hali, wakasaidiana na kupanana (peana) moyo. Hilo huleta mapenzi na mshikamano baina yao. Na iwapo pale pasomwapo maulidi Waislamu ni wachache, kutembelewa kwao na ndugu zao wanaotoka sehemu nyengine huwatia moyo, na pia huwafanya wahishimiwe na wale jirani zao wasio Waislamu.
  • Katika hayo, ni lipi la bid'a, kama hapana la sunna?

  • Kutangaza Uislamu na kusilimisha wengine: Katika Qur'ani Tukufu (Sura 5:67) Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume Wake (s.a.w.w.) awafikishie watu Ujumbe aliompa. Na katika khutba yake ya mwisho, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alituamrisha sisi wafuasi wake tuufikishe Ujumbe huo kwa yule ambaye haujamfikia. Na hilo limepatikana -- na linaendelea kupatikana -- maulidini kwa ushahidi wa rikodi ya wengi waliosilimu baada ya kuhudhuria maulidini na kusikiliza kaswida na khutba zinazotolewa huko.
  • Jee, bid'a ni ipi hapo?

  • Kumkumbuka Mtume Muhammad (s.a.w.w.): Qur'ani Tukufu (Sura 41:34) inatwambia kuwa jema na ovu si sawa. Ukitaka kuliondoa ovu, liondoe kwa jema ndipo ovu litakapofutika. Na Mtume (s.a.w.w.) naye ametwambia vivyo hivyo. Hali kadhaalika wazee nao wanatwambia kwamba tukitaka kumpokonya mtoto wembe ili asijikate, tusimwache mikono mitupu maana ataurudia. Badali yake tumpe kitu chengine kisicho na madhara (k.m mpira) ashike. Kwa njia hii tutamwokoa na madhara.
  • Katika zama kama hizi zetu ambapo Waislamu kwa jumla, na watoto wao khaswa, wanayajua zaidi ya viongozi wasio Waislamu, bali hata ya walio maadui wa Uislamu, katika nyanja mbalimbali, na husherehekea mazazi yao -- ni lipi bora? Tuwaache waendelee vivyo hivyo? Au tuwaambie waache kufanya hivyo bila ya kuwawekea badali yake? Au tuwawekee badali iliyo nzuri (ya sherehe za mazazi ya Mtume (s.a.w.w.) na viongozi wengine wa Kiislamu) ili tuwaachishe hayo waliyoyashika? Jawabu hapo ninakuachia wewe, ndugu Mwislamu.

    Mpaka hapa tumemaliza majibu yetu ya hujja zinazotolewa na wanaopinga maulidi; na kuwafikiwa ni kwa Mwenyezi Mungu.

    Inshallah wiki ijayo, kama tulivyoahidi katika makala yetu ya 9 Rabiuth Thani, 1423 / 21 Juni 2002, tutaanza kuyajibu ya Ahlu-Tawheed waliyoyasema katika makaratasi yao, "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulidi".