rudi maktaba >Maadili >Yaliyomo >

(4)

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Tunaendelea na hujja za wanaopinga maulidi na majibu yetu.

Katika hujja yao ya nne wanasema: Kwenye sherehe za maulidi hufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar (yanayochukiza, bali ni haramu kamwe, katika sharia ya Kiislamu).

MAJIBU YETU: Hiyo si hujja madhubuti. Kwa nini maulidi yote yatupwe kwa sababu tu ya kufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar katika sherehe zake? Kwa nini hayaondolewi hayo ya munkar, kama yako, yakabakishwa yasiyo ya munkar? Kwani tunda likiwa limeoza kidogo hutupwa lote, au hukatwa pale palipooza likaliwa pale pazuri palipobaki?

Katika hili tuna funzo zuri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yeye aliondoa tawafu ya Al-Kaaba, na Swafaa na Marwa, kwa sababu mwahali humo mulikuwa na munkar (masanamu) au aliamrisha yaondolewe hayo masanamu na watu waendelee kutufu? Tutaona kuwa Mwenyezi Mungu hakutuzuia kufanya jambo zuri lililokuwako (kutufu na kusa'yi) kwa sababu tu katika ibada hizo palikuwa na munkar (masanamu). Alilolifanya ni kuondoa munkar uliokuwako, akatuacha tuendelee na mazuri yaliyobaki (tawafu).

Kwa hivyo, kama katika maulidi kuna munkar wowote, la sawa ni uondolewe munkar huo, na maulidi yaachwe yaendelee. Si kumtupa jongoo na ung'ongo (ujiti) wake.

Kidokezo

Baada ya kutoa makaratasi yetu kwa wiki tatu, makundi mawili ya wanaopinga maulidi yamejitokeza. La kwanza limejita "Ahlu-Tawheed"; na la pili linajita "Wakereketwa wa Sunna Malindi". Na yote mawili hayakutoa anwani zao!

Ahlu-Tawheed wametoa makaratasi yenye jina la "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulid". Katika makaratasi hayo, wamenukuu baadhi ya madondoo ambayo -- kwa maoni yao -- ni shirki. Lakini hawakutueleza vipi kuwako madondoo hayo katika vitabu hivyo, hata kama yatakuwa ni shirki kweli, yanafanya maulidi yoyote mengine (yasiyo na hayo wanayoyaona wao kuwa ni shirki) hayafai kusomwa.

Wakereketwa wa Sunna Malindi, kwa upande wao, wametoa makaratasi yenye jina la "Chapa ya Kwanza (1): Majibu ya Abdillah Nassir". Katika makaratasi hayo, ambayo wameahidi kuendelea nayo, hawajazungumzia maulidi. Walilolifanya ni kunizungumza mimi binafsi -- kwa ya kweli na ya uwongo! Lakini na wao pia, kama wenzi wao, hawajatueleza vipi vyovyote vile vitakavyokuwa mimi binafsi -- iwe ni kwa wema ama kwa uovu -- ni hujja tosha ya kuyafanya maulidi yawe hayafai kusomwa! Pengine watalieleza hilo katika makala yao yatakayofuatia.

Hata hivyo si nia yangu, kwa sasa, kuyajibu makaratasi hayo kwa sababu kutatutoa nje ya mfululizo wetu huu. Nia yangu inshallah ni kuendelea kuzijibu hujja zao zote nilizozidondoa katika makaratasi yetu ya kwanza ya tarehe 4 Rabiul Awwal, 1423 / 17 Mei, 2002. Baada ya hapo ndipo nitakapojibu hayo yaliyomo katika makaratasi yao hayo.

Kwa hivi sasa, napenda kuwahakikishia wanaosoma maulidi kwamba yote waliyoyataja katika makaratasi yao mawili hayo tutayajibu kiilimu na kistaarabu, kama ilivyo dasturi yetu, na kama tulivyofanya mpaka sasa, pamoja na kuonyesha kwamba hayana mashiko.

Kwa hivyo, tunawaomba wale walionayo makaratasi hayo wayaweke, wangojee majibu yetu inshallah.