rudi maktaba >Maadili >Yaliyomo >

(3)

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Bado tunaendelea na hujja za wanaopinga maulidi.

Hujja yao ya tatu ni kuwa: kuweka ada ya kusoma maulidi ni kuigiza Wakristo walioweka siku ya Krismasi; na Mwislamu haruhusiwi kufanya hivyo.

MAJIBU YETU: Mwislamu hazuiliwi kufanya jambo kwa sababu tu linafanywa na Mkristo au kafiri yoyote mwengine. Analozuiwa ni kufanya jambo kama linalofanywa na Mkristo, au kafiri yoyote mwengine, linapokuwa linakwenda kinyume na mafunzo ya Kiislamu; na hilo sio linapofanywa na Mkristo au kafiri yoyote tu, bali hata linapofanywa na Mwislamu mwenziwe; haruhusiwi kulifanya.

Tunaposoma historia, kwa mfano, tunaona jinsi Bwana Mtume (s.a.w.w.) -- katika Vita vya Handaki -- alivyokubali shauri la Salman Farisi la kuchimba handaki kama walivyokifanya Wafursi kwao. Na Wafursi, wakati huo, hawakuwa ni Waislamu, bali walikuwa ni makafiri waliokiabudu moto! Jee, kwa kuwaigiza makafiri hao katika uchimbaji wa handaki, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alikosea?

Hali kadhaalika, tukija kwenye hijja mathalan, tunaona jinsi mahujaji wanavyokwenda baina ya Swafaa na Marwa, na jinsi wanavyochinja wanyama mwisho wa hijja yao. Lakini vitendo kama hivyo, kabla ya Uislamu, vilikuwa vikifanywa na makafiri! Basi kama kuigiza Wakristo hakuruhusiwi, kwa nini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) wakatuamrisha kufanya mambo ambayo dhahiri yake ni sawa na kuwaigiza makafiri?

Ukivizingatia vizuri vitendo hivyo utaona kwamba, japokuwa kwa dhahiri vinafanana na vile vya makafiri, kwa kweli huwezi kusema kuwa ni sawa na kuwaigiza makafiri. Kwa nini? Kwa sababu waliyokuwa wakiyafanya makafiri mwahali humo, walikuwa wakiyafanyia masanamu yao, waliyoyaweka humo. Kwa hivyo yao ilikuwa ni shirk (ushirikina). Lakini tunayoyafanya sisi Waislamu, baada ya kuondolewa mbali masanamu hayo, huwa tunamfanyia Mwenyezi Mungu Mmoja tu, asiye na mwenziwe (mshirika). Kwa hivyo yetu ni tawhid (kumpwekesha Mwenyezi Mungu).

Hali kadhaalika tunapokuja kwenye Krismasi. Japokuwa Krismasi, kama maulidi, hufanywa kwa kusherehekea mazazi ya Mitume ya Mwenyezi Mungu (Nabii Muhammad s.a.w.w. na Nabii Isa a.s.), lakini sherehe mbili hizo -- kama ambavyo kila mtu anajua -- si sawa. Sherehe zinazofanywa Krismasi ni tafauti kabisa na zinazofanywa maulidini, kama ambavyo Wakristo wanavyomchukulia Nabii Isa a.s. (Yesu Kristo) ni tafauti kabisa na vile Waislamu wanavyomchukulia Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Kwa mfano, Waislamu hawamchukulii Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuwa ni Mungu, wala ni Mtoto wa Mungu, wala ni Roho Mtakatifu.

Kwa hivyo kuwa tu jambo fulani lilitangulia kufanywa na makafiri -- wawe ni Wakristo ama ni wengineo -- haiwi ni hujja ya kuwazuilia Waislamu kulifanya jambo hilo maadamu watayatoa yote ya ukafiri yaliyokuwamo humo. Na hivyo ndivyo maulidi yalivyo. Zaidi ya kuwa zote mbili -- Krismasi na maulidi -- ni sherehe za mazazi ya Mitume ya Mwenyezi Mungu, hakuna jengine linalofanana katika sherehe hizo.

Kama tutashikilia kuwa ni haramu Waislamu kuwaigiza Wakristo, au makafiri wowote kwa jumla, katika jambo lolote -- hata kama halipingani na dini yetu -- basi sio wanaosoma maulidi tu, bali hata wanaoyapinga pia watakuwa makosani. Kwani ni nani kati yao aliyeacha gari au ndege, akaendelea kupanda punda, farasi au ngamia? Ni nani, anayejimudu, aliyeacha kutumia umeme (spaki), akaendelea na kuni au mafuta ya taa? Ni nani anayeradhiwa kujipepea kwa kipepeo au nguo yake, akaacha -- ikiwa anayo nafasi -- kutumia banka au AC (Air Conditioner)? Ni nani anayepanda kwa miguu mpaka ghorofa ya 15, au ya 10, akaacha lifti? Kwa nini hawayaachi yote hayo ili wasiwe wanawaigiza Wakristo au makafiri wengine, maana yote hayo yameanzishwa na wao.

Kwa hivyo si sawa kuwazuilia Waislamu kusoma maulidi kwa sababu tu ya kuwa, kufanya hivyo, ni kuwaigiza Wakristo katika sherehe zao za Krismasi.

Inshallah, katika makala yanayokuja, tutaijadili hujja yao ya nne.