rudi maktaba >Maadili >Yaliyomo >

(1)

WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU

Katika makala yetu ya kwanza tuliahidi kuzijadili ki-ilimu, moja baada ya moja, hujja zinazotolewa na wanaopinga maulidi. Kwa hivyo leo tunaanza:

Hujja yao ya kwanza ni kwamba: maulidi hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) Kwa hivyo, kuyaleta baada ya yeye kufariki dunia, ni bid'a (uzushi). Na kila bid'a, kwa maneno yake mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.w.), ni upotevu. Kwa hivyo, kila anayesoma maulidi amepotea!

MAJIBU YETU: Ni kweli kwamba maulidi, hivi tunavyoyasoma, hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Lakini si kweli kwamba, kulifanya kila ambalo halikuwako zama hizo, ni upotevu. Kama ni hivyo, basi bila shaka Waislamu wote leo -- wakiwamo wanaopinga maulidi -- wangelikuwa wamepotea kwa kuwa (katika zama zao mbalimbali) wamefanya, na wanaendelea kufanya, mambo ambayo hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)!

Kwa mfano, katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.), misikiti haikuwa ikitandikwa chochote (watu wakisujudu juu ya mchanga); lakini leo inatandikwa majamvi, busati na mazulia! Kiwanja kitakatifu cha Al-Kaaba kilikuwa ni mchanga mtupu na mawe; lakini leo kimetandikwa marumaru! Watu walikuwa wakenda kuhiji kwa kupanda ngamia au majahazi; lakini leo wanakwenda kwa ndege, meli za kisasa na mabasi ya anasa (luxury)! Watu, walipokuwa wengi msikitini, walikikhutubu kwa kupaza sauti zao; lakini leo wanatumia vipaza sauti (loud speakers)! Misahafu ilikiandikwa kwa mkono, juu ya ngozi na mifupa, na kutolewa nakala chache; lakini leo inachapwa kwa mashini, juu ya karatasi za fakhari, na kutolewa nakala mamilioni kwa mamilioni!

Lakini hakuna anayesema -- hata hao wanaopinga maulidi hawasemi -- kwamba Waislamu waliobuni mambo hayo wametuletea bid'a au wamepotea. Kwa nini? Kwa sababu kwao wao, na kwa wanaosoma maulidi, uzushi wa aina hiyo si bid'a; sio alioukusudia Bwana Mtume (s.a.w.w.). Alioukusudia yeye ni ule wa kuzua jambo katika dini hii ambalo halitokani nayo (maa laysa minhu). Hilo ndilo lililo wazi kutokana na Hadithi mashuhuri ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) inayosema: "Yoyote atakayezua, katika dini yetu hii, jambo ambalo halitokani nayo, litarudishwa (litakataliwa)."

Ukiitaamali vizuri Hadithi hiyo, itakudhihirikia kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w.) hakutuzuia kuzua (kubuni), katika dini hii, kila ambalo halikuwako zama zake. Kama angelitaka kutuzuia hivyo, Hadithi hiyo isingelisema hivyo, bali ingelisema hivi: "Yoyoye atakayezua jambo katika dini yetu hii, litakataliwa." Na lau ingelisema hivyo, basi yote yale tuliyoyataja hapo juu yasingeliruhusiwa; yangelikuwa bid'a.

Lakini Hadithi haikusema hivyo. Ilivyosema ni: " Yoyote atakayezua … ambalo halitokani nayo, litakataliwa." Kwa kuongeza kifungu cha maneno tulichokichapa kwa italiki (yaani "ambalo halitokani nayo"), ni wazi kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w.) hakukusudia kuwazuia Waislamu kufanya kila ambalo halikuwako zama zake. Alilolikusudia ni kutuachia wazi mlango wa kubuni mambo katika dini hii bora tu yawe yanatokana nayo.

Sasa suali hapa ni: jee, maulidi si katika mambo yanayotokana na "dini hii", hata kama hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)?

Majibu yetu ni: Maulidi, na yaliyomo maulidini, si mageni na "dini hii", bali yanatokana nayo, kama tutakavyobainisha kwa urefu zaidi katika majibu yetu ya hujja Na. (v) ya wapinzani wake inshallah.

Kwa hivyo, kuwa tu jambo halikuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) si hujja ya kuwazuia Waislamu kulifanya. Wanalozuiliwa Waislamu kulifanya ni kuzua jambo na kulifanya ni dini hali ya kuwa halina asili na dini. Na maulidi si hivyo!

Inshallah, katika makala yanayofuatia, tutaijadili hujja yao ya pili.