rudi maktaba >Maadili >

Maadili ya Kiislamu Katika Vita

Ustadh Shahid Murtadha Mutahhari

Mu'awiyah bin Abu Sufyan alikuwa akitawala Sham kama liwali karibu miaka 16. Katika kipindi hicho alikuwa akijitayarisha kushika ukhalifa bila ya kumwarifu mtu yeyote.

Alitumia kila fursa aliyoipata kutekeleza azma yake.

Kisingizio kikubwa alichopata ili kuiasi serikali kuu na kutangaza ukhalifa wake kilikuwa ni tukio la kuuawa Uthman.

Katika uhai wa Uthman, Mu'awiyah hakuyaitikia maombi yake ya kutaka kusaidiwa, kwani alikuwa akingoja auawe na atumie mauaji yake kama ni kisingizio cha kutekeleza njama yake.

Uthman aiipouawa, Mu'awiyah akatumia haraka fursa hiyo.

Kwa upande mwingine, baada ya kuuawa Uthman watu wakajikusanya kwa Ali (AS) kumbai, ambaye alikuwa akikwepa kuchukua dhima ya ukhalifa kwa sababu kadhaa.

Ali baada ya kuona kwamba hilo lilikuwa ni jukumu lake rasmi, akakubali, na ukhalifa wake uliokuwa rasmi ukatangazwa mjini Madina ambapo ulikuwa makao makuu ya Darul Khalifah (utawala) katika zama hizo. Mikoa yote ya dola kuu la Kiislamu katika zama hizo iliitii serikali kuu isipokuwa Sham (Syria) ambayo ilikuwa chini ya madaraka ya Mu'awiyah. Mu'awiyah akakataa kuitii serikali kuu na akaituhumu kwa kuwapa usalama (uhifadhi) wauaji wa Uthman, na akajitayarisha kutangaza uhuru wa Sham na Syria na kukusanya jeshi kubwa la Washamu.

Ali (AS) baada ya kuamua tatizo la watu wa Jamal, akamshughulikia Mu'awiyah.

Akaandikiana barua kadhaa na Mu'awiyah lakini barua za Ali hazikutia athari yoyote katika moyo mgumu wa Mu'awiyah.

Pande zote mbili zikapeleka majeshi yao makubwa katika uwanja wa vita.

Abul A'war as-Salami akaongoza jeshi la Mu'awiyah pamoja na kikundi cha watakadamu (watangulizi) na wakaingia katika medani. Na kwa upande wa jeshi la Ali, Malik Ashtar an-Nakhai akaongoza akiwa pamoja na maamiri jeshi kadhaa.

Vikundi viwili vya maamiri jeshi vikakutana ukingoni mwa Mto Furati. Malik Ashtar hakuruhusiwa na Ali kuanza vita.

Abul A'war akaanza kushambulia vikali kuonyesha ujasiri wake, lakini shambulio hilo likavurugwa na Malik Ashtar na wenzake na Washamu wakarudi nyuma.

Abul A'war akapanga njia nyingine kulishinda jeshi la Ali, na akaenda mahali paitwapo Shari'ah penye bonde karibu na Mto Furati. Majeshi yote mawili yalibidi yateke maji mahali hapo.

Akaamrisha askari wenye mikuki na mishale wahifadhi mahali hapo ili wawazuie Malik na watu wake.

Haukuchukua muda Mu'awiyah mwenyewe akaja pamoja na kikosi chake na akafurahishwa na utangulizi wa Abul A'war. Ili kuaminisha zaidi, Mu'awiyah akazidisha idadi ya askari wa Abul A'war, na wafuasi wa Ali wakawa na dhiki ya maji.

Kwa jumla, Washamu wakafurahi kupata fursa hiyo, na Mu'awiyah akasema kwa furaha:

"Huu ni ushindi wa kwanza."

Amr al-'Aas, msaidizi na mshauri mahsusi wa Mu'awiyah, peke yake ndiye aliyeona kwamba hakukuweko maslahi yoyote kuchukuliwa hatua hiyo.

Kwa upande mwingine, Ali (AS) alipofika na kupashwa habari juu ya jambo hilo akamwandikia barua Mu'awiyah na akampa Sa'sa'ah aliyekuwa miongoni mwa wafuasi wake wakubwa. Katika barua hiyo aliandika:

"Sisi tumekuja hapa lakini kwa vyovyote vile hatutaki vita vitokee na ndugu Waislamu wakauana wenyewe kwa wenyewe. Tunataraji tutaweza kuzitatua hitilafu kwa kufanya mazungumzo, lakini mimi nimeona kwamba wewe pamoja na wafuasi wako mmetangulia kushika silaha, na juu ya hivyo mmewazuia wafuasi wangu wasipate maji. Amrisha waache kitendo hicho ili tuanze mazungumzo. Bila shaka ikiwa wewe huridhiki na kitu kingine isipokuwa vita, basi jua kwamba mimi siogopi."

Barua hii ikafikishwa kwa Mu'awiyah, naye akashauriana na washauri wake kuhusu jambo hilo. Kwa jumla washauri wote walitoa maoni kwamba hiyo ilikuwa fursa nzuri sana ambayo hapana budi kutumiwa, na barua isijibiwe.

Lakini Amr al-'Aas peke yake ndiye aliyekuwa na maoni tofauti. Akasema: "Mnakosea. Kwa kuwa Ali na wafuasi wake hawataki kuanza vita na kumwaga damu ndiyo maana hivi sasa wamenyamaza kimya. Wamekuandikieni barua ili mbadilishe mawazo yenu.

Msifikiri kwamba mtakapoipuuza barua hiyo na mkawaweka vivyo hivyo katika shida ya maji wao watarejea. Hali ikiendelea kama hivyo watafuta panga zao na hawatosita mpaka watakapokufukuzeni mbali ya Furati na kukufedheheni."

Lakini washauri wengi walikuwa wakiamini kwamba kwa kuwanyima maji adui atashindwa na atalazimika kurudi nyuma. Mu'awiyah mwenyewe alikuwa akiafikiana na mawazo hayo.

Ushauri huo ukamalizika. Sa'sa'ah akarudi kwa Mu'awiyah kuchukua jawabu. Mu'awiyah akiwa na nia ya kurusha jawabu ya barua, akamwambia: "Nitajibu baadaye!"

Wakati huohuo akatoa amri askari walinde mto kwa uangalifu mkubwa na wawazuie askari wa Ali wasiingie wala wasitoke.

Ali (AS) akahamaki sana kuona kwamba haikuweko nia njema kutoka upande wa wapinzani na haikubaki njia nyingine ya kuwepo ufumbuzi kwa ajili ya mazungumzo.

Njia iliyobaki ilikuwa ni kutumia nguvu na silaha. Akaja mbele ya jeshi lake na akatoa hotuba fupi ya kusisimua na kutia hamasa:

"Hao wameanza uchokozi na wamefungua mlango wa ugonivi kwa kukupokeeni nyinyi kwa uhasama. Hao ni kama wato wenye njaa wanaotafuta chakula, hutafuta vita na umwagikaji wa damu.

"Sasa ni lazima mchague njia moja kati ya mbili, wala hakuna njia ya tatu. Ama mkubali madhila na unyonge na mbaki katika hali hii hii ya kiu, au mzishibishe panga zenu kwa damu zao chafu ili mtoe kiu yenu.

"Kuishi ni kushinda hata kuwe ni kwa kima cha kufa. Na kufa ni kushindwa na kutawaliwa hata kuwe ni kuishi vipi. Hapana shaka kwamba Mu'awiyah amewakusanya watu waliopotea na wasiofahamu na anatumia ujinga na upumbavu wao hata ikafikia kwamba maskini hao wanalengwa mishale ya mauti kutokana na ujinga wao."

Hotuba hiyo ya kusisimua imeleta msisimko wa ajabu katika jeshi la Ali. Damu zao zikachemka. Wakawa tayari kwa vita, na kwa kufanya shambulio moja kali wakawarejesha nyuma sana maadui na wakateka Shari'ah.

Wakati huo ambapo Amr al-'Aas alikuwa akitazamia kutokea jambo hilo, akamwambia Mu'awiyah:

"Sasa ikiwa Ali atalipiza kisasi na atakutendea kama wewe ulivyowatendea, utafanya nini? Utaweza kuikomboa Shari 'ah kutoka mikononi mwao?"

Mu'awiyah akauliza. "Kwa maoni yako sasa Ali atatufanyia nini?"

Amr al-'Aas akasema. "Nionavyo mimi, Ali hatolipiza kisasi na wala hatotunyima maji. Yeye hakuja hapa kwa kazi hiyo."

Kwa upande mwingine, baada ya askari wa Ali kuwakimbiza mbali wafuasi wa Mu'awiyah kutoka katika Shari'ah, wakamwomba Ali awaruhusu wawazuie wafuasi wa Mu'awiyah wasichote maji. Ali (AS) akasema:

"Msiwazuie. Mimi ninapinga mwendo huu wa wajinga. Mimi nitaitumia fursa hii kuanza mazungumzo nao kufuatana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ikiwa watakubaliana na mapendekezo yangu na ufumbuzi wangu itakuwa ni afadhali, lakini wakikataa, basi nitapigana nao kwa ushujaa na wala si kwa kuwafungia maji maadui."

Kisha Ali (AS) akaongeza kusema: "Mimi sitofanya mambo hayo kamwe na wala sitomdhikisha mtu yeyote kwa maji."

Kabla ya kuingia usiku, askari wa Ali na Mu'awiyah walikuwa wakienda kwenye mto huo kuchota maji, na hakuna mtu aliyemzuia hata askari mmoja wa Mu'awiyah.