Muhimu wa Hijab

 

Kimeandikwa na:

Sayyid Saeed Akhtar Rizvi

 

Kimetafsiriwa na:

Dhikiri U M Kiondo

 

 

UTANGULIZI

 

Neno “Hijaab” ni neno Ia Kiarabu lenye maana ya kisetiri, pazia, buibui, mtandio, au ushungi. Neno hili limetumika katika Qur'ani Tukufu kwa maana ya kuwatenga wanawake kutokana na wanaume wanaoweza kuoana nao, lakini hawakuoana nao (wanaume walio Ghair-Mahram wao).

 

Hivyo, kwa wanawake wa Kiislamu, kutochanganyika na wanaume wageni na kuvaa buibui au ushungi watokapo nje ya nyumba zao, ni amri ya Mwenyezl Mungu, wala si lo lote lile miongoni mwa yale wanayoyafikiria wajinga au yale wanayoyasema maadui wa Uislamu; kama tutakavyoona katika hotuba hii.

 

Hotuba hii ilitolewa katika Semina ya nane ya "Golden Crescent Group" iliyofanyika mjini Lushoto mnamo tarehe 22/10/1977.

 

Kiini cha Uislamu ni "Kujitoa kabisa ili kutimiza Penzi la Mwenyezi Mungu", kuzifanya fikara na mwelekeo wa mtu kuwa wenye kuzitii Amri za Mwenyezi Mungu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

­Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke

aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao; Na mwenye kumwasi Mwenyezl Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi". (Qur’ani, 33:36).

 

Hivyo basi, kama utauliza ni kwa nini Hajaab ni wajibu, jibu pekee liwezalo kutolewa ni, kwa sababu Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameamua hivyo. Na ni lazima huo uwe mwisho wa hoja zote kwa kadiri mwanamume aliyeamini na mwanamke aliyeamini wahusikavyo.

 

Katika zama hizi, Hijaabu imelinganishwa na kutoendeIea kwa jamii na inafikiriwa kuwa ni ishara ya kifungo cha wanawake. Wahubiri wengi wanafikiria kuwa ni bora kutolizungumzia jambo hili katika majlisi zao. Lakini Mtukufu Mtume (s.a.w.) amesema: “Inapotokea Bidaat na mwanachuoni asikiseme kile akijuacho (dhidi ya Bidaat hiyo), basi (mwanachuoni huyo) hulaaniwa na Mwenyezi Mungu, malaika na wanadamu.”

 

IsIamu ni dini thabiti ambayo ndani yake sheria zote na taratibu zote vimerekebishwa vizuri na kama mtu anataka kugeuza sehemu fulani, utaratibu wote utaharibika. Ni lazima uukubali muundo mzima kama ulivyo. Huwezi kuchagua la ku­chukua na la kuacha kutoka katika muundo huu.

 

Uislamu unaamini kuwatenganisha wanaume na wanawake.

Umewapa wanaume na wanawake madaraka tofauti kabisa, kutegemeana na uwezo wao wa kimaumbilee Mwanaume ana­wajibika kutafuta mahitaji ya maisha kwa ajili yake na jamii yake. Mwanamke amepewa madaraka ya kusimamia mambo ya nyumbani, na kulea watoto chini ya misingi ya Kislamu.

 

Watetezi wa uhuru wa wanawake huudhihaki mgawanyo huu wa kazi, wakidai kuwa malezi mazuri ya watoto ni kazi duni yenye kuwashusha cheo wanawake. Hawatambui kuwa mpango wao mpya wa kijamii, unaowanyima watoto malezi na uangalizi wa wazazi ndio sababu kubwa ya kuongezeka kwa makosa ya watoto, jambo ambalo baadaye huipasua pasua jamii.

 

Hijaab, kama tuijuavyo, haikuwepo Uarabuni kabla ya Uislamu. llianzishwa na Mtume (s.a.w.) mjini Madina baada ya kuteremshwa amri maalum za Qur’ani Tukufu, miaka mingi kabla ya kusilimu kwa watu wasio Waarabu.

 

Ummul-Muuminiin, Bibi Aisha alikuwa kila mara akiwa­sifu wanawake wa Kiansar (wa Madina) kwa maneno haya "Baraka za Mwenyezi Mungu ziwashukie wanawake wa Kian­sar. Mara baada ya kuteremshwa Aya za Sura ya An-Nur waliacha kutoka nje (ya nyumba zao) kama walivyokuwa wakifanya kabla ya hapo. Walianza kuvifunika vichwa vyao kwa nguo nyeusi, kana kwamba kunguru alitua vichwani mwao".

 

Hadithi nyingine yenye maana hii hii imepokewa kutoka kwa Umuul-Muuminiin, Bibi Umu Salma.

 

Hivyo basi, jitihada za baadhi ya Makafiri waliojifanya kuwa ni wajuzi sana wa Uislamu ya kuonyesha kuwa Hijaab iliuingia Uislamu Waarabu walipoziteka nchi jirani, hazina maana hata kidogo. Haya ni mojawapo ya misingi ya sheria za Kiislamu. Mtukufu Mtume (s.a.w.) amesema: "Kuwa na haya ndio Uislamu".

 

AYA YA HIJAAB

 

Kwanza, hebu ngoja tuzisome Aya za Qur'ani Tukufu zinazohusu jambo hili. Ziko Aya tatu katika Sura ya An-Nur.

 

(1-2) Aya mbili za kwanza ni hizi

 

"Waambie waaminio wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao; bila shaka Mwenyezi Mungu Anazo habari za yale wanayoyafanya.

 

"Na waambie waaminio wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe "Ziinat" (mapambo) yao …. Ma Dhwahara Minha” (Isipokuwavaie yalivodhihirika katika hayo); na waangushe “Khumur” (shungi) zao mpaka “Juyuub” (vifuani) mwao, na wasionyeshe “Ziinat” (mapambo) yao ila kwa ….. me wao, au wana wao, au wana wa waume wao, au umbu zao, au wana wa maumbu wao, au wana wa dada zao, au wanawake wao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au watu wafikao mara kwa mara wasio watamanifu katika wanaume, au watoto ambao hawajajua siri za wanawake; wala wasipige miguu yao ili yajulikane wanayoyaficha katika mapambo vao; na tubieni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi waaminio, ili mpate kufaulu. (Qur'ani, 24:3O-31).

 

Maelezo ya Maneno Muhimu:

 

(i)         Ziinat:

 

Ziinat: Ni kile mwanadamu akitumiacho kujipambia kama vile mapambo, nguo na vitu kama hivyo.

 

(ii)        Khumur:

 

Kwa 'Khumur' zao, yaani kwa shungi zao, wingi wa ‘khimar' ambalo maana yake ni ushungi; unaitwa hivyo maana unafunika kichwa.

 

(iii)      Juyuub:

Wingi wa Jaib; yaani mfuko wa shingo. Kabla ya kuteremshwa Aya hii, wanawake wa Kiarabu hawa­kuwa na kawaida ya kufunika shingo zao na kwa kawaida mishipi ya shingo ilikuwa chini (walijitwalia mtindo wa karne ya ishirini… "). Hivyo waliamrishwa kufunika shingo zao kwa shungi zao.

 

(iv)             Mahram:

Orodha ya ndugu ambao mwanamke anaruhusiwa kuwaonyesha Ziinat zake inatolewa katika Aya hii. Ndugu hawa wanaitwa "Mahram". Maana ya Mahram na wale ndugu (wa kuzaliwa, kulea au wa ndoa) ambao ndoa kati yao na mtu huyo imekatazwa daima. Hivyo, baba wa mumewe mke au mkwe ni "Mahram”; lakini dada wa mkeo si Mahram, maana unaweza kumuoa baada ya kufariki mkeo (au baada ya kumtaliki mkeo).

 

Neno "baba zao" hujumlisha ami (baba mdogo au baba mkubwa) na amu (mjomba).

 

(v)               Illa Ma Dhwahara Minha:

 

"Isipokuwa yale yaliyodhihirika katika hayo". ltaelezwa baadaye.

 

(3)               Aya nyingine katika Sura hiyo hiyo inamsamehe mwanamke mzee sana kuvaa ushungi.

 

"Na Al-Qawaaid (wanawake wazee) ambao hawatumaini kuolewa, basi si viabaya kwao “Ya lwa-ana” (kufunua) nguo zao (za kujifunika usoni) bila kuonyesha mapambo; na kama wakichelea ni bora kwao; na Mwenyezi Mungu ni Asikiaye, Ajuave. (Qur’ani, 24:60).

 

Maelezo ya Maneno Muhimu

 

(vi) AI-Qawaaid: Ni wale wanawake waliokwisha pita umri wa kuingia katika hedhi (damu ya mwezi) na nifas (damu ya uzazi) na si wenye tamaa zandoa kwa sababu ya uzee wao.

 

(vii) Ya lwa-ana: Neno hili halina maana ya kuvua vazi (kama vile shati n.k.) kutoka mwilini. Lina maana ya kulaza upande nguo ya nje (kama vile ushungi au blanketi). Hadithi moja inaelezea kuwa “Ataulaza upande Mharuma (Shaliau kashida) au nguo ya kujifunikia kwa nje).”

 

Tofauti hii hudhaniwa kuwa ndio sheria yenyewe kwa ujumla. Wanawake wazee wanaweza kulaza upande shungi zao au "Burqa” inaonyesha kuwa wengine hawaruhusiwi kulaza upande shungi zao. Na hata hao wanawake wazee wameombwa kutolaza upande shungi zao kwa maana ni bora kwao na (pengine kutoa mfano mzuri kwa kizazi kidogo).

 

Na ziko Aya Nne katika Sura ya Al-Ahzab:

 

Mbili katika hizo ni hizi

 

Enyi wake wa Nabii, ninyi si kama ye yote katika wana­wake mkimcha (Mungu), basi msiwe laini katika usemi ili asitamani mtu mwenye ugonjwa moyoni mwake, na semeni kauli njema. Na kaeni majumbani mwenu, wala msionyeshe mapambo sawa na maonyesho ya ujinga wa zamani; … (Qur'ani, 33:32-33).

 

Maelezo ya Maneno Muhimu:

 

(viii) Wake wa Nabii: Aya hii inazungumza na wake wa Nabii

lakini wanawake wote wa Kiislamu wamejumlishwa ndani yake; kama vile aya nyingi sana zinazozungumza na Mtukufu Mtume (s.a.w.) zina maana ya kuzungumza na Ummah mzima. Kwa mfano iko aya isemayo:

 

"Ewe Nabii! mtakapotoa talaka kwa wanawake; basi toeni talaka katika wakati wa eda zao..." (Qur'an1, 65:1).

 

Ni imani ikubaliwayo kabisa kuwa sheria za Qur'ani ni kwa Ummah wote ila pale panapoeleza wazi wazi kuwa si kwa watu wengine.

 

(ix) Ninyi si kama ye yote katika wanawake:

 

Wanawake wa Kiislamu si kama wanawake wa kifakiri. Hivyo ni lazima watunze cheo chao.

 

(x)        Sawa na Maonyesho ya Ujinga wa Zamani:

 

"Kukaa majumbani mwenu” ni heshima ya Uislamu; na kujionyesha ni alama ya biashara ya zama za Ujinga na Kufuru.

 

(5)       Aya ya tatu yao ni hii

 

“…..Nanyi mnapowaomba (wakeze Nabii Muhammad s.a.w.) basi waombeni nyuma ya pazia; hayo ni safi kabisa kwa mioyo yenu na kwa mioyo yao... (Qur'ani, 33:53).

 

Maelezo ya Maneno Muhimu:

 

(xi) Aya hii vile vile inazungumza na wakeze Mtukufu Mtume (s.a.w.). Inaonyesha wazo la Hijaab kwa mwanamke wa Ki­islamu, kuwa ni lazima abakie nyumbani mwake; na wanaume Ghair Mahram wake wazungumze naye inapokuwa lazima tu; na inapobidi kuzungumza nae, wazungumze naye nyuma ya pazia linalowafanya wasionane.

 

Ilipoteremshwa Aya hiyo hapo juu, Sahaba mmoja alimu­uliza Mtume (s.a.w.) kama iliwabidi Waislamu kujificha wasi­onwe na binti zao, mama zao, na maumbu wao pia. Hapo ndipo ilipofunuliwa aya hii ifuatayo:

 

(6)       Aya yenyewe

 

"Si dhambi juu yao (wanawake) katika (kuonana na) baba zao, wala watoto wao, wala umbu zao, wala wana wa dada zao, wala wanawake wao, wala wale iliyowatamalaki mikono yao ya kuume; Mwogopeni Mwenyezi Mungu (enyi wanawake); bila shaka Mwenyezi Mungu ni Shahidi juu ya kila kitu (Qur’ani, 33:55).

 

Hivyo, swali aliloliuliza yule Sahaba likawa limejibiwa.

 

(7) Aya ya mwisho katika Sura hii ni hii

 

"Ewe Nabii, waambie wake zako na mabinti zako na wake wa waaminio wateremshe juu yao "Jilbaab" (shungi) zao; ili wajulikane wazi wazi na wasiudhiwe; na Mwenyezi Mungu. Ni Msamehevu, Mrehemevu. (Qur'ani, 33:59).

 

Maelezo ya Mameno Muhimu:

 

(xii) Jalabib: Neno "Jalabib" ni wingi wa neno "Jilbaab".

 

Jilbaab ni joho kubwa kuliko ushungi na fupi kuliko Mha­ruma (shari au kashida) ambalo mwanamke hulivaa kichwani na kumfunika mpaka kifuani...

 

Na inasemekana kuwa "Jilbab" ni blanketi na aina zote za mavazi zifunikazo mwili kama vile mharuma n.k. Na maana ya ni kuwa, ni lazima wateremshe mitandio juu ya miili yao ili izifunike nyuso zao na mabega yao.

 

Aya hizi zinawaongoza wanawake kama ifuatavyo:

 

(a)       Ni lazima wakae majumbani mwao.

 

(b)       Wasiseme kwa maneno laini wanaposema na watu Ghair-Mahram waoe.

 

(c)        Ni lazima liwepo pazia mlangoni.

 

(d)       Wasionyeshe "Ziinat" zao ila kwa wale Mahram wao.

 

(e)       Kama ikiwabidi kutoka nje ya majumba yao (kwa sa­babu ya haki) waifunike miili yao kwa mitandio.

 

Kutokana na Aya hizi zote, inaonyesha kuwa ziko hatua mbili za Hijaab (a) Hijaab ya Macho na (b) Hijaab ya nguo.

 

HIJAAB YA MACHO:

 

Wanaume walioamini wateremshe macho yao chini, na wanawake walioamini ni lazima wateremshe macho yao chini. Hakuna aruhusiwaye kumtazama mtu asiye wa umbile lake (la kiume au la kike), ila tu awapo Mahram wake.

 

Kwa kuwa mwanaume ameamriwa kujitahidi kutafata mahitaji ya maisha, hakuambiwa kuficha mwili wake (ila kwa kiwango Fulani tu). Vivyo amelazimihwa kuteremsha macho yake chini na kutowatazama wanawake wasio mahram wake..

 

Ziko hadithi nyingi sana zisemazo:

 

"Tazamo (la jicho) ni mshale wenye sumu utokanaona mshale wa Shetani".

 

"Hakika kutazama kunakotokana na Shetani".

 

"Jihadharini na kutazama."

 

Ye yete yule ayajazaye macho yake kwa (kutazama vitu) Haram, (yaani watu wasio Mahram) Mwenyezi Mungu atayajaza macho yake kwa Moto ila tu anapotubia na akarudi (kwenye Uchamungu.

 

Hadithi nyingi sana zaeleza kuwa tazamo jingine baada ya tazamo Ia kwanza ni mshale wa Shetani na ni Haramu".

 

HIJAAB YA NGUO:

 

Tunaweza kulijadili jambo hili chini ya vichwa vya habari vifuatavyo:

 

1 KIWANGO CHA KUJIFUNIKA:

 

Vazi hilo ni lazima liufunike mwili mzima wa mwanamke, iIa zile sehemu zilizosamehewa. Kufuatana na hadithi sahihi za vitabu vya Kishia na Kisunni, “mwili mzima wa mwanamke ni Awrah”.

 

Kwa mfano katika hadithi hii ifuatayo tunaambiwa:

 

“Hakika wao (wanawake) ni ‘awrah’.

 

Mwanamke ni ‘awrah’.

 

Nini maana ya neno "awrah"?

 

“Via vya uzazi vinaitwa "awrah" kwa sababu ni aibu ku­vitazama; na kila kitu ambacho mtu hukificha (kwa sababu ya fahari au aibu) kinaitwa "Awrah”; na wanawake ni “Awrah”.

 

Kufuatana na maelezo ya kitabu kiitwacho "Al-Urwatul ­Wuthqaa" kilichoandikwa na Sayyid Kadhim Yazdi, chenye maelezo chini ya kurasa yenye majina ya Mujtahid wote wa­liohai, kuna aina mbili za mitandio:

 

(1)       Kwanza: ni ule mtandio ulio Wajibu wakati wote:

 

Huu ni

 

(a)                Kuficha Awratain (sehemu za siri, nyuma na mbele) kutoka machoni pa watu wote, wanaume na wanawake, Mahram, na Ghair-Mahram, Wa­liobalehe na wasio balehe.

 

Tofauti: Mume na mke wanaweza kutazamana. Vile ile mtoto mdogo sana amesamehewa kuifuata amri hii.

 

(b)               Kwa vile ni Haramu kuzifunua sehemu hizi za mwlli mbele ya mtu ye yote yule, basi ni Haramu kuzitazama.

 

(c)                Ni wajibu kwa Mwanamke kujifunika mwili mzima (ila uso na mikono yake hadi kwenye vifundo vya viganja jambo ambalo tutalieleza baadaye) kutoka machoni pa watu wote ila mumewe na Mahram wake.

 

Uso na mikono:

 

(i) Kiasi upo uwezekano wa mtu fulani kumtazama kwa ashki, basi itakuwa wajibu kufunika uso na mikono pia.

 

(ii) Kama hakuna uwezekano huo, basi itakuwa ‘Ahwat’ (ni bora) kuzifunika sehemu hizo kwa mujibu wa Fatwa ya Sayyid Mahmuud Husaini Shahrudi, Sayyid Abul Qasim Khui, Sayyid Muhammad Kadhim Shariatmadari, Sayyid Muhammad Redha Gulpaygani na sayyid Hadi Milani.

 

(iii) Ni haramu kutazama kwa ashki mwili uso au mkono wa mume au mke, awe Mahram au Ghair- Mahram (Ila kwa mume na mkewe).

 

(2)       Aina ye Pili ya Mtandio inahusu Sala:­

 

(i) Mwanaume ni lazima afunike Awratain zake hata kama hapana mtu wa kumtazama. Na ni Ahwat kuifunika sehemu ya mwili iliyo baina ya kitovu na magoti.

 

(ii) Mwanamke ni lazima afunike mwili wake mzima pamoja na nywele na masikio ila uso (tangu paji la uso hadi kidevu, kwa urefu ni sehemu yote ya uso yenye upana wa tangudole gumba hadi kidole cha katikati) mikono (tangu vifundo vya kiganja hadi ncha za vidole) na miguu mpaka penye vifundo vya mikono. Ni wajib kufunika sehemu ya zile sehemu zilizosamehewa katika amri hii “Min Babil Maqaddamah”.

 

(iii) Si lazima kwake kufunika mapambo yake wakati wa sala au sehemu za uso zilizokwatuliwa.

 

(iv) Kama yuko mtu anayeutazama au atakayeweza kuutazama kwa ashki uso wake, mikono yake au miguu yake wakati wa Sala,  basi itamuwajibikia kuzifunika sehemu hizi vile vile, si kwa sababu ya Sala, bali kwa sababu ya Sheria nzima iliyotajwa kabla kwa ujumla.

 

2.         USO NA MIKONO

 

Katiika aya ya kwanza imeelezwa kuwa wanawake wasidhihirishe ‘Zinat' (mapambo) zao ila "Ma Dhwahara Minha" (yale yaliyodhihirika katika hayo)”.

 

Kuna kutoafikiana kuhusu maana ya haya mapambo yali­yosamehewa kufichwa.

 

Kipo kikundi (katika Madhehebu za Kisunni na Kishia) kisemacho kuwa maana ya kifungu cha maneno kisemacho? “Ma dhwahara Minha" ni uso na mikono, sehemu ambazo kufua­tana na maoni yao, mwanamke anaruhusiwa kutozifunika. Ili kuikubali tafsiri hii, ni lazima mtu ajendeleze maana ya neon “Zinat” kujumlisha "uzuri wa kimaumile.”

 

Kikundi kingine kinasema kuwa kifungu hiki "Ma Dhwa­hara Minha" kina maana ya yale matukio ambapo sehemu yoyote ya mwili wa mwanamke au pambo linaonekana kwa ajili ya sababu zisizozuilika kama vile kuvuma kwa upepo, au nguo za nje zenyewe.

 

Tukiachilia mbali hadithi za Masunni, ziko Hadithi nne katika vitabu vya Kishia ambazo wazi wazi au kiundani ndani zinaiunga mkono tafsiri ya kwanza.

 

Hadithi ya kwanza imesimuliwa na Bwana Mardak bin Abid ambaye alisikia kwa mtu fulani aliyemsikia Imamu Jaafar Sadiq (a.s.) akisema kuwa haya mapambo yanayoweza kuachwa wazi ni: uso, mikono na miguu (chini ya vifundo).

 

Hadithi ya pili imesimuliwa na Bwana Qasim bin Urwah aliyeisikia kutoka kwa Imamu Jaafar Sadiq (a.s.) aliyesema kuwa ina maana ya wanja na pete (ikiwa na maana ya macho na mikono).

 

Hadithi ya tatu imesimuliwa na Bwana Sadan bin Muslim aliyemsikia Imamu Jaafar Sadiq (a.s.) akisema kuwa mapambo haya yawezayo kuachwa wazi ni pete na bangili (ikiwa na maana ya mkono tu).

 

Sasa yule mtu katika hadithi ya kwanza, Bwana Qasim bin Urwah katika hadithi ya pili na Bwana Sadan bin Muslim ka­tika hadithi ya tatu ni watu wasiofahamika kabisa. Hakuna ajuaye mabwana hawa ni nani, ni kiasi gani twaweza kuyate­gemea maneno yao.

 

Hadithi ya nne imesimuliwa na Bwana Amr bin Shimr aliyeisikia kutoka kwa Bwana Jabir bin Ansar, kuwa Bwana Jabir alisema kuwa alikwenda pamoja na Mtume (s.a.w.) nyu­mbani kwa Fatima (a.s.) na akamuona (Bibi Fatima) ame­pauka. (Yaani Bibi Fatima a.s.) hakuufunika uso wake n.k.

 

Huyu Amr bin Shimr alikuwa muongo mkubwa na wana­vyuoni wa Kisunni na Kishia wanasema kwa pamoja kuwa ali­kuwa na desturi ya kubuni hadithi na kuzihusisha na Mabwana Jabir, Jufi na wengineo.

 

Zaidi ya hapo hadithi hii inakwenda kinyume na hadithi zikubaliwazo zithibitishazo kuwa Bibi Fatima (a.s.) alikuwa akijifunika kabla ya kumruhusu Sahaba mmoja kipofu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.) kuingia nyumbani mwake, na kuwa hakupenda jeneza lake kuwekwa katika ubao usiofunikwa (kama ilivyokuwa kawaida ya zama hizo) kwa sababu watu watajua urefu wake.

 

(Hivyo oni lililo sahihi ni lile la kikundi cha pili, lisemalo kuwa maana ya maneno “­Dhwahara Minha” ni yale matukio tu ambapo kiungo cha mwili au pambo hufunuka ajili ya sababu zisizozuilika).

 

Hata hivyo, ni tofauti za kimaandishi tu. Tukija kima­tendo Wanavyuoni wote (kwa pamoja) wanasema kuwa kama ipo hatari ya watu kumtazama mwanamke usoni kwa nia mbaya, basi ni wajibu wake mwanamke huyo kuufunika uso wake. Na kufuatana na wasemavyo wengine, ni "Ahwat”.

 

Sasa ni juu yenu kuamua kati ya Mwenyezi Mungu na ninyi wenyewe kama ipo hatari hiyo katika hii jamii iliyopata mwanga.

 

3. UZITO

 

Hiyo nguo ni lazima we nzito vya kutosha ili isiweze kuionyesha rangi ya ngozi ya mwili au umbile la mwili.

 

Ni lazima tuwakumbushe wanawake wetu kuwa shabaha ya Hijaab si kuvaa nguo “yo yote” bali ni kuficha mwili. Nguo zionyeshazo au zilizo nyembamba zinazoonesha rangi ya ngozi ya mwili au umbo Ia mwili si Halali.

 

Kama vile Mtukufu Mtume (s.a.w.) alivyosema: "Katika zama za mwisho watakuwepo wanawake (Kasiyatin Ariyatin) watakaovaa nguo lakini wakabakia uchi. Kwa hakika hao wamelaaniwa.

 

Mtukufu Mtume (s.a.w.) siku moja alimuona bibi arusi aliyevaa nguo nyembamba na akasema: "Si mwanamke aiaminiye Sura ya An-Nur yule avaaye nguo ya aina hii".

 

4. KUPWAYA

 

Nguo hiyo isibane kiasi cha kuonyesha umbile la mwili wa mwanamke.

 

5. NGUO YA JUU IPASIKAVYO KUWA:

 

(a) Shabaha ya kuvaa nguo hii ya juu ni kuficha "Zinat". Hii inaonyesha kuwa hii nguo ya juu yenyewe isiwe ya aina inayoweza kuwavutia watazamaji kwa upande wa nguo za ndani za mwanamke. "Zinat" haziwezi kufichwa na nguo zifanyazo watu waelekeze macho yao kwa mvaaji. Ni aina hii ya nguo iliyokatazwa na aye hii ya Qur'ani:

 

“…­Wala msionyeshe mapambo sawa na maonyesho ya ujinga wa zamani.....” (Qur'ani. 33:33)

 

(b) Wanawake wasivae nguo ambazo kwa ujumla zinafahamika kuwa kwa kawaida huvaliwa na wanaume. Mtukufu (s.a.w.) amewalaani wanaume wafanyao mambo kama wanawake na wanawake wafanyao mambo kama wanaume.

 

(c) Isiwe nguo ya sifa, fahari na upuzi. Kuvaa nguo zakupendeza sana ili kujionesha hali ya mtu, nguo chafu sana, au nguo zilizokunjana kunjana ovyo ili kuonyesha jinsi mtu asivyojijali, au mtu kuzikataa kanuni za jamii hairuhusiwi. Kujionyesha na fahari ni mambo yasiyofaa katika Uislamu na hayapendwi na Akhlaq za Kiislamu Mtukufu Mtume (s.a.w.) alisema: "Ye yote yule avaaye nguo ya sifa katika ulimwengu huu Mwenyezi Mungu atamvisha nguo ya aibu katika Siku ya Kiama, ambayo imewashwa moto.

 

UMUHIMU WA HIJAABU:

 

Ili kuona jinsi Hijaab ilivyopewa umuhimu katika Sheria za Kiislamu, inatosha kutazama jinsi Sheria na amri nyingineno zinavyorekebishwa na kubadiliwa ili kuihifadhi sheria ya Hijaab:

 

(1) Kusali msikitini ni bora kuliko kusali nyumbani Thawabu huongezeka kwa kadri jamaa iongezekavyo.

 

Lakini kwa wanawake ni kinyume na hivi, Kuna Thawabu nyingi kuswali nyumbani kuliko kuswalia msikitini, na ni thawabu zaidi kuswali katika chumba cha ndani zaidi kuliko kuswali katika baraza au ukumbi.

 

(2) Sala ya Jamaa: Mojawapo ya misingi ya Sala ya Jamaa ni kuwa pasiwepo “Hayil (kuzuizi) kati ya Imamu na Maamuma na kati ya maamuma mmoja na mwigine.

 

Lakini amri hii si kwa wanawake. Kama wakitaka ku­swali kwa Jamaa, ni lazima wasali nyuma ya “Havil”.

 

(3) Adhana na Iqamah: Kuadhini na Kukimu vimetiliwa mkazo sana kabla ya sala tano za faradhi. Lakini wanawake wamesamehewa kuadhini na kukimu. Kama wakitaka kufanya hivyo wanaweza kufanya iwapo hapana mtu asiye Mahram wao awezaye kuzisikia sauti zao. Au sivyo itakuwa Haram kwao kufanya hivyo (Ingawa wanaweza kufanya hivyo kwa kunong’ona).

 

(4) Ni wajibu kwa wanaume kusoma Alhamdu na Sura katika rakaa mbili za mwanzo za sala ya Alfajiri, Magharibi na Isha kwa sauti.

 

Wanawake wanatakiwa waswali zote kwa kunung’ona.

 

(5) Sala ya Ijumaa ni Wajibu Aini anapokuwepo Imamu au Naibi wake aliyemteua, na ni Wajibu Ain au Wajib Takhyiri wakati wa Ghaibat kufuatana na Fatwa na Ulama wengi.

 

Lakini Mwanamke amesamehewa wajibu huu.

 

(6) Ghusl-i-Mayyit: Ni lazima mwoshaji awe Mwislamu, lakini kama mwanamke Mwislamu atakufa na wako Wa­naume Waislamu wasio Mahram wake na Wanawake wa Kikristo, basi ni Iazima yule mwanamke wa kikristo aombwe aoge kisha amuoshe yule maiti wa kike wa Kiislamu.

 

Mwanachuoni mwingine Muhaqqiq Hilli hakubaliani na maoni hava. Yeye anasema kuwa Ghusl-i-Mayyit ni Ibada na inahitaji kutia Nia na Nia ya Kafir si sahihi. Hivyo badala ya kuwaruhusu Waislamu wa Kiume kumuosha, anasema kuwa ni Iazima huyo maiti azikwe bila Ghusl.

 

(7) Kuna thawabu kubwa kuchukua Jeneza la maiti wa Kiislamu na kutembea katika msafara wa maziko.

 

Wanawake wamesamehewa kushiriki katika shughuli hizi.

 

(8) Katika Ihram, mwanamke haruhusiwi kufunika uso wake, lakini kama alivyoandika Bwana Muhaqqiq Thani Karki sheria hii inahusiana na Ihram wala haihusiani na kuwaona watu wawio Mahram wake.

 

Ayatullah Abul Qasim Khui ameandika kuwa mwanamke apendapo kujificha kutokana na watu wasio Mahram wake katika Ihram, anaweza kuvutia chini pembe ye Ihram yake katika uso wake na kidevu chake; lakini ni Ahwat kuwa aweke mkono wake au kitu kingine; chochote badala ye kuiweka nguo hiyo usoni mwake.

 

(9) Jihad, kupigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni Ibada ipendwayo zaidi.

 

Wanawake hawaruhusiwi kushiriki katika Ibada hii.

 

Hivyo tunaona kuwa kila Sheria ya kawaida inapopingana na Sheria ya Hijaab, si hijaab itoayo njia. Kila mara ni ile inayopingana na Hijaab ambayo hutolewa mhanga kwa ajili way amri ya Hijaab.

 

MASWALI NA MAJIBU

 

Sehemu hii ni ya maswali na majibu ya maswali yaliyoulizwa baada ya hotuba iliyotolewa katika Semina hiyo ya "Golden Crescent Group" iliyofanyika mjini Lushoto mnamo tarehe 22 Oktoba 1977.

 

Swali 1:          Je inaruhusiwa kwa Msichana aliyevaa ushungi kusoma katika Shule za Mchanganyiko (za Wavu….. na Wasichana)?

 

Jibu: Iwapo msichana huyo atazifunika sehemu zote za mwili ila uso na vitanga vya mikono (toka vifundo vyo kitanga hadi ncha za vidole), basi itaruhusiwa.

 

Swali 2:          Kama jibu ni "Ndio”, basi hataweza kujibu maswali atakayoulizwa na mwalimu, je, itambidi anong’one?

 

Jibu: Kuzungumza na “Ghair Mahram” (mtu asiyekuwa Mahram yako) huwa haramu kama itakuwepo hatari kuwa “Ghair Mahram” huyo atapata ashki kutokana na kuisikia sauti ya mwanamke huyo.

 

Swali 3:          Je, mwanamke aneweza kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii na kiuchumi akiwa kajitanda ushungi?

 

Jibu: Ndio, ilimradi asivuke mipaka iliyowekwa na Sheria ye Kiislamu. Kumbuka kuwa sehemu sahihi kwa mwanamke

ni ndani ya mipaka ya nyumba yaku tu.

 

Swali 4: Katika jamii nyingimume na mkw, wote wawili

ni lazime wafanye kazi. Kwa mfano katika jamii ya wakulima, kama illvyo nchini Tanzania, mume na mke, wote wawili ni lazima wafanye kazi ka­tika shamba ambalo, bila ya kulishughulikia familia yao itakufa njaa. Nini ushauri wako kuhusu hali hii?

 

Jibu: Kama mnataka kuufuata Uislamu nilazima muubadili utaratibu huu. Kwa hakika wazo la kuwa katika jamii ya kiukulima lazima mwanamke afanye kazi shambani limetokana na kutoangalia vizuri. Tunawaona wanawake wakifanya kazi nchini Tanzania na kishia tunajumlisha tu kuwa ni msingi wa kijamii. Tunasahau kuwa nchi zinazoulisha ulimwengu kama vile U.S. A., Canada, Australia n.k. ni nchi za Kilimo, lakini kilimo chao hakitegemei wanawake kufanya kazi ma­shambani. Hivyo, si kilimo kinachowataka kazi ya kuvunja migongo wanawake; bali  hali ya kuwa watu wako nyuma sana ndiyo inayowalazimisha wanawake wa Kitanzania kufanya kazi mashambani, si jamii ya kikilimo isababishayo hi­vyo. Na tunaweza kuseme kuwa Uislamu hauipendi hali hii ya kuwa nyuma katika maendeleo. Uislamu unawataka hawa wanawake warudi kwenye nafasi yao maalum, ambayo ni nyumbani. Kwa maneno mengine, jamii ya Kitanzania itawaji-bikiwa kutumia misingi ya Kiislamu iwapo inapenda kusonga mbele.

 

Swali 5:          Wanachuoni we Kiislamu wameamrishwa kuipinga "Bidat". Ni katika hatua ipi wanapotakiwa kufanya hivyo? Katika hatua ya mwanzoni au ya mwishoni?

 

Jibu:   Katika kila hatua.

 

Swali 6:          Wanawake wa Kiislamu katika nchi tofauti tofauti hujifunika shungi za aina tofauti tofauti. Ni aina gani ya shungi iliyo sahihi kufuatana na misingi ya Kiislamu?

 

Jibu: Aina yo yote ile itakayowapendezea ilimradi to iwawezeshe kuzifuata sheria za Kiislamu barabara; yaani waifiche miili yao.

 

Swali 7: Je, si lazima kwa wanawake wetu kwenda kujipatia elimu va utabibu na elimu ya kufanyiza madawa n.k.? Mwanamke mgonjwa atapendelea ugonjwa wake uchunguzwe na daktari wa kike kuliko wa kiume. Vile vile anaweza kujieleza vizuri bila ya kizuizi cho chote kile kwa mganga wa kike kuliko kwa mganga wa kiume. Viko vyuo vya utabibu vya wanawake viwili tu duniani, na kwa sababu ya uhaba wa madaktari wa kike, ni lazima kwa wanawake wetu kwenda kujiunga katika vyuo vingine na hivyo ni lazima wavue shungi zao.

 

Jibu: Ni lazima kwa mwanamke kujaribu kwenda kwenyi vyuo vya wanawake tu, sio katika vyuo vya mchanganiko. 

 

Swali 8:          Wanawake wengine wamefaulu kulinda heshima zao bila ya kuvaa shungi. Sasa kwa nini wanawake wajitaabishe kuvaa shungi na kumbe wanaweza kujipatia heshima zao hata bila ya kuvaa shungi?

 

Jibu: Ni lazima kwa wanawake wa Kiislamu wote. Heshima ya mwanamke wa Kiislamu mbele ya Mwenyezi Mungu hutegemea kuvaa kwake ushungi; kwa mfano, itazame Aya hii isemayo:

 

‘ninyi si kama wanawake wengine ….” Ni cheo na heshima ya wanawake wa Kiislamu “kukaa majumbani mwenu”. Kama tukijaribu kuitenga heshima yao na “Hijaab”, basi sura yetu haitapatana na sura alivyokusudia Mwenyezi Mungu.

 

Swali 9:          Ninaamini kuwa katika Uislamu, mume na mke watahesabiwa kuwa ni sawa katika Siku ya Hukumu. Sasa ikiwa ni hivyo, kwa nini katika hali hii ya sasa, ya kukua kwa hali ya maisha, mwanamke asifanye kazi na kumsaidia mumewe katika kuendesha maisha ya nyumbani?

 

Jibu: Msifuje mali na jaribuni kubakia ndani ya mipaka ya Uislamu. Mwanamke anaweza kumsaidia mumewe katika kuongezea kipato cha nyumba kwa njia zile tu, ambazo hazimlazimishi kutoka nje ya nyumba yake. Usawa katika Siku

ya Hukumu hauna maana ya kushiriki sawa katika kujipatia gharama za maisha katika ulimwengu huu.

 

Swali 10: Je, wazazi waache kumlazimisha bint yao kuvaa 'Hijaab', ili isimuwiye vigumu anapolazimishwa na watu wa upande wa mumewe kutoivaa?

 

Jibu: Unapokuwanaye timiza wajibu wako na madaraka yako.

Yatakayotokea baada ya anapokuwa na mumewe si wajibu wako.

Kama unachelea kuwa baada ya juma moja hutapata chakula

cho chote, je, utaanza kufa njaa tangu leo?

 

Swali 11:        Je, ni heshima kwa msichana kuvuliwa ushungi wake na watu wa upande wa mumewe?

 

Jibu:   Hapana. Ni haramu. Ni lazima kwa msichana huyo kukataa.

 

Swali 12:        Hijaab ni wajibu kwa msichana, lakini kama mu­mewe akimkataza kufanya mambo yaliyo wajibu, basi msichana huyu afanye nini? Je, ni wajibu kwa msichana huyu kumtii mumewe?

 

Jibu:   Hapana. Ni lazima asimtii mume huyo iwapo atamwa­mbia kufanya dhambi. Na mume anapata dhambi maradufu kwa kumlazimisha mkewe kuvua “Hijaab” au kufanya jambo lo lote lililo haramu.

 

Swali 13: Kufuatana na swali la 12 hapo juu, je, msichana huyo anaweza kuomba apewe talaka?

 

Jibu: Ndio, aneyo haki ya kuomba talaka iwapo mume huyo atamlazimisha kutovaa Hijaab. Lakini itukiapo hivyo, Muj­tahid ataamua kufuatana na hali ilivyo. Kwa mfano itambidi

atosheke kuwa huyu mwanamke halitumii hili swuala la Hijaab kwa hila au njia tu ya kujipatia taIaka.

 

Swali 14:        Tukiwa tuishakubali kuwa nafasi ya mwanamke ni nyumbani mwake, je, ni haki kumruhusu mwanamke wa nchi za kimagharibi kufanya kazi ili amsaidie mumewe ambaye kipato chake peke yake hakiwatoshi?

 

Jibu: Nadhani ni lazima kwanza jambo moja Iieleweke wazi wazi kabla ya kulijibu swali hili mojawapo ya madhambi makuu saba ni kama mtu anaishi mahali ambapo yu huru kabisa kuabudu dini aipendeyo, na anahamia mahali ambapo hatakuwa huru kuweza kuyafuata maamrisho ya dini, kunaitwa ……… (maana yake hasa  ni Kuhamaha­ma baada ya Hijrat). Ndugu zetu wengi imewabidi kuhamia nchi za Magharibi kwa sababu wasizoweza kuzizuia.  Hatu wezi kuwalaumu. Lakini wako wengine waliochagua tu kwenda kuishi katika nchi za Magharibi kwa sababu ya faida za kidunia. Wao wanayo madaraka makubwa, si kwa Akhera yao tu, bali vile vile kwa watoto wao na vizazi vyao vya baadaye.

 

Sasa tukilijia lile swali, ushauri wa kwanza wa watu wa namna hiyo ni kuwa wasiende katika nchi za namna hivyo ambako hawawezi kujipatia maisha yao bila ya kipato cha mke. Kama wanaishi katika nchi hizo na kwa sababu zisizozuililka basi mwanamke anaweza kufanya kazi nyumbani mwake ili kuongezea kipato cha mumewe. Lakini ni lazima azifuate barabara sheria zote za Kiislamu zinazohusu Hijaab.

 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.