Maadhimisho ya Maulid : 11th Rabbiul Awwal 1421 (4th June 2001)

Shaikh Akmal Hussein Tahiri (Bukoba)

 

Hotuba hii imetarjumiwa na Amiraly M.H.Datoo

 

 

Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu  Sura Aali Imran,  3, Ayah ya 164 :

 

Hakika Allah swt amewafanyia hisani kubwa Waislamu alivyowaletea Mtume miongoni wao, anayewasomea Aya zake, na anawatakasa na kuwafundisha Kitabu na hikima. Na bila shaka kabla ya hapo walikuwa katika upotofu dhahiri.

 

Kuhusu kutakasa nafsi : vitu sita: Adl, Sabr, Taqwa, Tawba, Hayaa, Sakhii

 

Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema kuwa vitu sita vinatakasa nafsi ya mwanadamu navyo ni mema kwa wote lakini bora kabisa kwa ajili ya watu sita, nao ni  :

1.       Adl  Uadilifu ni nzuri kwa ajili ya wote lakini ni bora kabisa kwa ajili ya mfalme au mtawala na lau mfalme au mtawala hatakuwa na uadilifu basi mfano wake ni sawa na wingu lisilo na maji ya kunyesha mvua. Hivyo wingu lisilo na maji ya mvua yanafaida gani ardhini wakati ni pakavu ?

2.       Sabr  ni nzuri kwa wote lakini ni bora kabisa kwa masikini na mafukara kwani mfano wa masikini au fukara asiye na subira ni sawa na taa isiyo na mwanga.

3.       Taqwa ni nzuri na muhimu kwa wote lakini ni bora kabisa kwa ajili ya Ma’ulamaa na ‘Aalim asiye na taqwa ni mfano wa mti usio na matunda ambao watu hawaufaidi.

4.       Tawba ni nzuri kwa wote lakini ni bora kabisa kwa ajili ya vijana. Na kijana asiye na Tawba ni mfano wa mto usio na maji. Hebu fikiria kuwa kuna mto lakini hauna maji, je unafaida gani ?

5.       Heshima ni nzuri kwa wote, lakini ni bora kabisa kwa ajili ya wanawake kwani mfano wake ni sawa na chakula kisicho na chumvi. Yaani utamkuta ni mwanamke lakini amekosa zile adabu za mwanamke. Iwapo kuna mtu ambaye amekosa ubinadamu, je huyo ataitwa mwanadamu ?

6.       Moyo wa kutoa  ni nzuri kwa wote lakini ni bora kabisa kwa ajili ya wenye utajiri na uwezo kwani tajiri asiye na moyo wa kutoa ni sawa na nyumba isiyo na paa.

 

Lakini ndugu zangu Mtume Muhammad s.a.w.w. vile vile ametuonya tujitahadharishe na vitu 3 ambavyo vitateketeza mema hayo ya juu na ambavyo vitatufikisha hata Jahannam (Motoni).. Navyo ni:

 

1.       Al-Kibr Kiburi ni kitu kibaya kabisa yaani ni hali ya roho ya mwanadamu ambamo mtu huwa na hisia ya kujiona yu bora zaidi ya wengineo na mienendo yake huwa ya ufakhari. Kibr kinatokana na mtu kuwa na pesa, mali, cheo, ilimu, watoto na hata maumbile na urembo.  Mtume Muhammad s.a.w.w.  amesema : “Kamwe hataingia mtu Peponi aliyenaye hata kiasi cha chembe cha kiburi moyoni mwake”

2.       Al-‘Ujb inajumuisha kujipenda na majivuno. Mtu anapojiona kuwa mwenzake amekipata kama chake basi  huingiwa na huzuni wakati ambapo anatakiwa amwombee mwenzake apate zaidi na yaliyo mazuri zaidi.

3.       Su’ al-Khalq Kukosa adabu kwa watu. Hivyo inatubidi kuwa na kauli nzuri pamoja na matendo yetu yawe mema kiasi cha kuwashinda maadui zetu bila ya mapigano. Sisi sote tunafahamu kisa cha Mtume Muhammad s.a.w.w. kuwa alikuwa akitupiwa takataka na kutandaziwa miiba na mwanamke wa Kiyahudi. Lakini Mtume Muhammad s.a.w.w. alipoona kuwa siku zimepita bila ya kufanyiwa maovu hayo, aliulizia na akaambiwa kuwa yule mwanamke alikuwa akiumwa, na hivyo Mtume Muhammad s.a.w.w. alikwenda kumjua hali, mwanamke alipomwona Mtume Muhammad s.a.w.w. alidhani kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amekwenda kulipiza kisasi lakini Mtume Muhammad s.a.w.w. alimwambia kuwa yeye alikuja kuuliza hali yake ya ugonjwa. Kwa tabia hii njema ya Mtume Muhammad s.a.w.w. mwanamke huyo alisimu bila mapigano. Ama kwa tabia njema za Mtume Muhammad s.a.w.w. hata Qur'an Tukufu  inatoa ushahidi kuwa ‘yeye ni bora kwa tabia njema’

 

Hivyo kwa munasaba huu wa kuadhimisha siku ya uzawa huu mtukufu wa Mtume Muhammad s.a.w.w. ninapenda kutoa salaam zetu zenye furaha kwa ‘Ummah mzima wa Kiislamu na wiki hii nzima iwe ni wiki ya ‘umoja na upendo miongoni mwetu’ na nawaomba vijana na ndugu zangu wote turudi katika dini ya Islamu na tufuate mienendo ya Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa upendo vile tunavyoaadhimisha uzawa wake huu mtukufu.

 

Mawaidha mengi mmeyasikia na mutayasikia kutoka kwa Masheikh mbalimbali ambayo yanatosheleza kwetu sisi kupata miongozo ya Dini.

 

Wabillahi Tawfiq,

Wassalaam ‘alaykum wa Rahmatulahi  Ta’ala wa Barakatuhu.

 

Shaikh Akmal Hussein Tahiri,

Jumuiya ya Shia’ Ithna’Ashariyyah

BUKOBA.

 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.